Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Njombe
WAZIRI wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akiwa Mkoani Njombe hivi karibuni amesema kuwa, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa miradi miwili mikubwa ya kufua umeme wa jumla ya megawati 580 kwa njia ya maji ambayo ni, Mradi wa Ruhudji na Mradi wa Rumakali yote kwa pamoja ikiwa mkoani Njombe.
Ameeleza kuwa,Mradi wa Ruhudji utazalisha megawati 358 na Mradi wa Ruamakali utazalisha megawati 222 ambapo maandalizi ya ujenzi wa miradi hiyo miwili mikubwa yameanza utekelezaji wake kwa wakati mmoja ikiwemo maandalizi ya Miundombinu wezeshi kwaajili ya ujenzi rasmi wa miradi hiyo.
“Utekelezaji wa miradi hii ulianza kwa hatua ya kufanya usanifu wa Miradi tangu Desemba 2020 na unakaribia kukamilika. Sasa tunatarajia kuingia hatua ya pili ya kutangaza zabuni ili kuwapata wakandarasi kuanzia mwezi Machi ili ifikapo mwezi Julai wakandarasi wawe wamepatikana na tuwakabidhi rasmi eneo la ujenzi ili waweze kuendelea na ujenzi,”amesema Waziri Kalemani.
Waziri Kalemani ameongeza kuwa, miradi yote miwili inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu na hivyo kuongeza megawati 580 katika Gridi ya Taifa ili kuongeza uwezo ambapo kwa sasa Grid ya Taifa ina uwezo megawati 1602 tu.
“Kwa mahitaji ya sasa, Nchi nzima tuna uwezo wa kutumia mpaka Megawati 1400, lakini kadri tunavyoongeza umeme katika Gridi, ndivyo tunavyo hamasisha na kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi toka nje na ndani ya Nchi, hivyo Serikali imeamua kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi hii miwili ya Ruhudji na Ruamakali,”amesema Waziri Kalemani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya ameushukuru uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kuanza kutekeleza miradi hiyo muhimu kwa Taifa ambayo utafiti wake ulifanyika miaka mingi iliyopita, lakini haikufikia hatua ya utekelezaji.
Rubirya ameongeza kuwa, mbali na miradi hiyo kuwa na manufaa makubwa kwa taifa, lakini ni matarajio ya wananchi wa Njombe kuwa, miradi hiyo itafungua fursa za uwekezaji mkubwa katika Mkoa wa Njombe na maeneo ya jirani.
“Niihakikishie Serikali, Wizara ya Nishati na TANESCO kuwa, Mkoa wa Njombe utaendelea na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ya kutunza mazigira ambayo yatawezeha upatikanaji wa maji kwanza kwajili ya Mradi Mkubwa wa Julius Nyerere lakini pia Miradi hii ya Ruhudji na Ruamakali,”amesema Rubirya.
Kwa upande wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Uzalishaji Umeme, Mhandisi Pakaya Mtamakaya alisema sambamba na miradi hiyo ya kufua umeme zitajengwa njia mbili za kusafirisha umeme huo za Msongo wa Kilovolti 400.
“Njia ya kwanza itajengwa kutoka Ruamakali hadi Kituo cha Mwakibete Mbeya na ya pili kutoka eneo la Ruhudji mpaka kilipo kituo cha kupoza umeme Mkoani Iringa ili kuwezesha usafirishaji wa umeme huo kuingia katika Gridi ya Taifa na kutumika katika mikoa mbalimbali nchini,”amesema Mhandisi Pakaya.
Akimalizia ziara yake mkoani Njombe, Waziri Kalemani ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe kujiandaa kupokea miradi yote miwili pamoja na kuchangamkia fursa zote za kujipatia kipato kutokana na ujenzi wa miradi hiyo huku akiwasihi wananchi wa Mkoa wa Njombe kulinda vyanzo vya maji, kutunza mazingira pamoja na miundombinu yote ya umeme.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi