Na Mwandishi wetu, Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI imepanga kujenga majengo ya kiuchumi katika majiji ya Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nairobi ghorofa 22.
Kupitia mpango huo Serikali itajenga DRC jengo la ghorofa 25 na Kenya ghorofa 22.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh241.069 bilioni ambapo kati ya fedha hizo sh. bilioni 229.4 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. bilioni 11.6 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Makamba, Serikali ina nyumba na viwanja 109 dunaini kote na kodi ya pango wanayolipa ni sh bilioni 29 kwa mwezi.
Amesema uwekezaji huo ukikamilika utaingiza sh. bilioni 36 kwa mwezi na kwa mwaka sh. bilioni 692.
“Wizara imeingia nakubaliano ya ubia na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Nairobi,” amesema.
Amesema mradi huo unahusu kuendeleza kiwanja kilichopo katika eneo la Upperhill jijini Nairobi kwa kujenga majengo pacha ya ghorofa 22.
Makamba alisema Wizara imekamilisha taratibu za kisheria za makabidhiano ya nyaraka na kuhamisha rasmi majukumu ya ujenzi wa mradi kwenda NSSF.
“Wizara pia kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imekamilisha maandalizi ya nyaraka za kisheria kwa mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi Kinshasa DRC.
“Utekelezaji wa mradi huo unafanyika katika kiwanja cha ubalozi kilichopo mtaa wa Boulevard de 30 Juin jijini Kinshasa ambapo utahusisha ujenzi wa jengo la ghorofa 25.
Amesema pia Wizara inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya majengo ya Wizara pamoja na vitega uchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi