Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali inaandaa Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam unaolenga kutoa suluhisho la changamoto zilizopo katika jiji hilo ambao utekelezaji wake utaenda sambamba na usimamizi wa uendelezaji miji kwa kuzingatia matumizi yaliyoainishwa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula leo Jijini Dar es Salaam alipokutana na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaa kujadiliana juu ya mpango huo lakini pia zoezi zima la ukwamuaji urasimishaji katika jiji hilo.
Waziri Mabula aliongeza kuwa kila mamlaka ya upangaji inao wajibu wa kisheria kuweka mkakati wa kuzuia uendelezaji usiofuata sheria, kanuni na taratibu akiongeza kuwa bila kufanya hivyo serikali itashindwa kutekeleza mipango iliyowekwa na hivyo kutumia fedha za wananchi vibaya.
Waziri Mabula ameongeza kuwa Dira ya Mpango Kabambe ni kuwa na Jiji endelevu, lenye ushindani linalotumia rasilimali zake kiufanisi na kuhifadhi mazingira na unaolenga kukukuza utamaduni na kuhifadhi historia yake ya muda mrefu.
Waziri Mabula aliwambia wajumbe wa Mkutano huo kuwa Mpango umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya 2025 iliyofafanuliwa katika Mpango wa Maendeleo wa 2021-22 hadi 2025-26 na unatoa mwongozo katika utoaji wa maamuzi katika matumizi na maendelezo ya Ardhi ili kuhakikisha uendelezaji wenye mpangilio katika ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam hadi mwaka 2036.
Aidha Waziri Mabula ameongeza kuwa Mpango huo unatoa majibu ya changamoto zinazolikabili Jiji ikiwemo msongamano wa magari, ujenzi holela, uhaba wa huduma za jamii na miundombinu.
‘’Mapendekezo ya Mpango Kabambe huu yamezingatia uongezaji wa fursa za uwekezaji ambao mwisho wa siku utaongeza ajira kupitia miradi mbalimbali iliyopendekezwa,, Alibainisha Waziri Angeline Mabula.
Dkt, Mabula alitaja baadhi ya miradi iliyopendekezwa kuwa ni Ujenzi wa viwanda maeneo ya Pugu, Pembamnazi, Kisarawe II na Kimbiji, Ujenzi wa barabara ya mzunguko katika Manispaa za Ilala na Ubungo, Uboreshaji na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi.
Miladi mingine ni uhifadhi wa maeneo ya kihistoria katikati ya Jiji, Mradi wa maji safi katika eneo la Kimbiji, Ujenzi wa madampo la kisasa katika maeneo ya Kisopwa na Lingato, Ujenzi wa viwanda vidogo vidogo katika baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa urasimishaji.
‘’Hadi sasa urasimishaji makazi nchini umefanyika katika Mitaa 1961 katika halmashauri 164 za Mikoa yote 26. Katika mitaa hiyo jumla ya viwanja 2,338,926 vimebuniwa kupitia michoro ya mipangomiji 7,051’’. Aliongeza Waziri Mabula.
Waziri Mabula pia ameongeza kuwa Suala la upimaji nalo limefanyika kwa kiasi kikubwa ambapo jumla ya viwanja 1,170,639 vimepimwa na kuidhinishwa ambavyo ni sawa na asilimia 50.4 ya viwanja vyote vilivyopangwa.
Kukamilika kwa Mpango Kabambe huu kumekuja wakati muafaka, pamoja na kutumika kama chombo cha kuongoza na kusimamia uendelezaji wa Jiji na kudhibiti ujenzi holela, pia utatoa uhakika kwa wawekezaji katika Jiji hili, utaondoa changamoto mbalimbali zikiwemo za migogoro ya matumizi ya ardhi, ukuaji wa makazi yasiyo rasmi, uharibifu wa miundombinu, uharibifu wa mazingira na kukuza fursa za uwekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi