November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuja na mkakati endelevu kudhibiti uvuvi haramu

Na Mbaraka Kambona,TimesMajira online,Kigoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mpango wa kuwa na mkakati endelevu wa kudhibiti uvuvi haramu na kuachana na utaratibu wa kuendesha oparesheni za muda mfupi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi ambapo alisema kuwa Serikali ipo katika mipango ya kuandaa mkakati shirikishi na endelevu wa kupambana na uvuvi haramu nchini. Ndaki alifanya Mkutano na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliopo Mkoani Kigoma

Ndaki amesema hayo wakati akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi ulipo katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma Aprili 24, 2021.

Akiongea na wavuvi hao Ndaki alisema kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwa na udhibiti wa uvuvi haramu ambao utakuwa endelevu utakaoshirikisha wahusika wenyewe wanaofanya shughuli za uvuvi na viongozi wa eneo husika kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa.

Sehemu ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakifuatilia matukio yanayoendelea katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma

“Tunataka kuja na mkakati endelevu wa namna ya kudhibiti uvuvi haramu, tuusike sote, kuanzia Wataalamu, Viongozi wa ngazi zote na wananchi wanaohusika na uvuvi wenyewe,” alisema Ndaki huku akiongeza kuwa

“Uvuvi haramu unatishia rasilimali zetu za uvuvi, tusiulee, tuwashirikishe wahusika ili waone kuwa uvuvi haramu ni kitu kisichokubalika” amesema.

Kwa Mujibu wa Ndaki amesema walichokigundua katika mkakati wa kutumia oparesheni za muda mfupi ni kwamba matokea yanakuwa ya muda mfupi na operesheni hizo zikiisha matukio ya uvuvi haramu yanaendelea tena kwa sababu operesheni hizo zinahusisha wataalamu kutoka Wizarani na sio wahusika wenyewe wa eneo husika.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) Katika Mkutano wa Waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma

‘‘Ulinzi wa rasilimali za uvuvi sio jukumu la watu wa makao makuu peke yake, ni jukumu letu sote, tuone umuhimu wa kutunza rasilimali zetu na wote tukubaliane kuwa uvuvi haramu haukubaliki na tukikukamata sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Ndaki

Kuhusu baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu alisema kuwa kiongozi au mtaalamu yeyote mwenye dhamana ya masuala ya uvuvi atakayepatikana kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu na yeye atakuwa haramu na atashughulikiwa kama wahalifu wengine.

Ameongeza kuwa kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia masuala ya uvuvi na eneo lake linafanya uvuvi haramu, wataanza kumchukulia hatua huyo kiongozi na wengine wote watakaokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kwa kutokuwajibika kwao.

Ndaki amesema kuwa hatalegeza nati hasa linapokuja suala la uvuvi haramu na kuwataka wananchi na viongozi wa ngazi zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita uvuvi haramu huku akiwahimiza kuwafichua wale wote wanaohusika na vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.