November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuimarisha mahusiano na sekta binafsi Rukwa

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha mahusiano kati ya sekta ya umma na binafsi yanaimarika ili kukuza uzalishaji ajira na uchumi  kupitia fursa mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Rashid Mchatta jana wakati akifungua kikao cha majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi Manispaa ya Sumbawanga .

Mchatta alisema ukuaji uchumi unaongozwa na sekta binafsi katika kuzalisha ajira na fursa za kiuchumi endelevu hususan kwa vijana na kuwezesha serikali kupata mapato kupitia kodi na ushuru wa bidhaa .

“Serikali inaweka mazingira wezeshi kwa sekta ya binafsi katika ukuaji wa biashara kubwa ,ndogo na makampuni.  Kikao cha hiki kinalenga kujadili fursa,mafanikio na changamoto zinazoikumba sekta binafsi” alisema Mchatta.

Kwa upande wake Mshauri wa Sekta Binafsi toka Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma Awamu ya Pili (PS3) Moses Kabogo iliyoratibu kikao hicho alisema lengo ni kujenga mahusiano mazuri kati ya sekta ya umma na binafsi.

Kabogo aliongeza kusema mradi huo unajikita katika kuhakikisha jamii iliyoko pembezoni inafikiwa kiurahisi kupitia sekta bianfsi ambapo changamoto zinatatuliwa kupitia majadiliano.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Rukwa Willington Kiziba alitoa wito kwa serikali kutazama upya mifumo yake utoaji bima ya afya ili kuwezesha makundi yote kwenye jamii kufikiwa na huduma kwa gharama nafuu.