November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuboresha mitaala vyuoni kuhusu Sekta ya madini

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

SERIKALI ipo mbioni kurekebisha mitaala ya elimu kwa vyuo vikuu na vya kati ili kutengeneza wataalam wa kutosha na wenye ushindani mkubwa watakaoweza kuhudumia Sekta ya Madini nchini.

Hayo yamesemwa leo na Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo jijini Dodoma, katika mahojiano maalum na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Madini.

Amesema, katika kutafsiri Maono ya mwaka 2030, Madini ni Maisha na Utajiri, na kuelezwa kuwa wizara hiyo imeamua kuongeza nguvu katika nyanja ya uboreshaji wa tija kwa watumishi pamoja na watoa huduma katika sekta ya madini.

Hata hivyo amesema, katika kusimamia ushirikishwaji wa Watanzania kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini, Serikali itashirikiana na Kampuni zilizowekeza katika sekta hiyo hapa nchini, ili kujua uhitaji wao kwenye huduma wanazopatiwa na Watanzania katika miradi yao.

“Tunashirikiana na kampuni hizi ili kujua nini wanahitaji, ili tuboreshe mitaala kwenye vyuo vyetu, kuanzia vyuo vikuu hadi vyuo vya kati vinavyofundisha mitaala hiyo, tunataka tuwe na mitaala ya kimataifa ili wakitoka mafunzoni wakatoe huduma stahiki, wapate uzoefu na waelewe kazi kivitendo,” amesema Janet.

Pia, amesisitiza kuwa Serikali imepanga kuwaangalia Watanzania ambao walifanya kazi hapa nchini na kwenda nje ya nchi kufanya kazi kama wataalamu kupata taarifa zao ili waweze kurejea kwenye kampuni zilizopo kwa lengo la kufundisha Watanzania, ujuzi waliojifunza katika nchi tofauti.

Aidha, ameongeza kuwa lengo la wizara kufikia 2030 ni kuhakikisha huduma stahiki inatolewa kwa maboresho ili kuongeza tija kupitia wataalam wa ndani na nje ya nchi, kwa watumishi na wafanyakazi kwenda nje kujifunza au kuleta wataalam kuja kuwafundisha wafanyakazi hapa nchini.

“Kwa kuangalia kazi zilizopo na kuangalia huduma tunayotoa kwa wateja wetu, tunahitaji kutoa huduma kwa kiwango gani katika kila kazi iliyopo kwenye muundo wetu, tuongeze nini kwa kuangalia mapungufu yaliyopo ili kuongeza tija, tunahitaji wataalam wazawa wenye uwezo mkubwa na viwango vya kimataifa,” amesema Janet.

Sambamba na hilo, pia amesema njia nyingine ni kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa utoaji huduma stahiki kwa kuangilia mataifa yaliyopiga hatua zaidi katika utoaji huduma kwa kuangalia wapi wamefanikiwa zaidi ili kuongeza tija.

Katika kikao Cha Wachimbaji Wakubwa na Wadogo kilichofanyika Oktoba 27, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Kamishna Janet alidokeza mambo kadhaa ambayo Serikali imepanga ikiwa ni maandalizi ya Tanzania kuhakikisha inashiriki ipasavyo katika uchumi wa Madini Mkakati na Muhimu.