November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuandaa sera ya kushirikisha wazawa katika miradi ya kimkakati

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji Geoffrey Mwambe amesema katika kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika kuwawezesha Wananchi kushiriki katika shughuli za Kiuchumi, Serikali kupitia Ofisi hiyo ipo mbioni kuikamilisha Sera ya Taifa ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji (National Local content Policy).

Itakumbukwa mnamo mwezi Juni mwaka huu, katika mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,aliiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji kutengeneza kwa haraka Sera ya Taifa ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji.

Waziri Mwambe alisema, kwa sasa serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya Kimkakati na Uwekezaji, ili kuhakikisha ushiriki wa wananchi na makampuni ya watanzania unakuwa mkubwa katika miradi hiyo, serikali imeamua kuwepo kwa sera itakayo wezesha jukumu la kuratibu, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa masuala ya local content katika ngazi ya kitaifa.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Sera ya Local content utasaidia Upatikanaji wa ajira na uendelezaji wa nguvukazi ya wananchi wa Tanzania, itawezesha urithishaji ujuzi na teknolojia. Aidha, kutakuwa na uhakika wa ubia kati ya makampuni ya Tanzania na wawekezaji.
Mhe. Mwambe emeeleza kuwa serikali imedhamiria wananchi kushiriki katika shughuli za uchumi katika maeneo muhimu Uziduaji (Madini, Mafuta na Gesi), Ujenzi, Usafirishaji na Mawasiliano Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Biashara, Utalii na Sayansi na Teknolojia.

Akiwa katika ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya uwekezaji, shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mwambe aliweza kufanya mashauriano ya namna bora ya kuzitatua changamoto zinazowakabili wawekezaji katika viwanda ikiwemo; SANDVICK services Ltd, Alpha choice Ltd, Omega Fish Ltd, Victoria Polybags Ltd, Prince Pharmaceuticals Ltd,Tangreen Agriculture Limited na Busolwa Mining Ltd.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji Geoffrey Mwambe akisisitiza jambo wakati alipotembelea Prince Pharmaceticals Ltd, Kiwanda cha Mwekezaji mzawa cha kuzalisha Dawa aina 28 na chakula nyongeza (Glucose) moja, jijini Mwanza, Kulia kwake ni mkuu wa mkoa huo, Robert Gabriel.