Na Martha Fatael, timesMajira online
SERIKALI mkoani Kilimanjaro imeweka mikakati ya udhibiti wa rasilimali za maji na uharibifu wa vyanzo vya maji ili kukabiliana na hofu ya kutoweka kwa raslimali hiyo kwa miaka ijayo kama inavyotahadharishwa na wataalamu wa maji nchini.
Kadhalika mkoa huo unatarajia kujiwekea mikakati ya kiubunifu ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ambayo hupotea ili kukabiliana na upungufu wa maji inayoongezeka karibuni kila mwaka.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameyasema hayo wakati akifungua kikao Cha kwanza Cha jukwaa la wadau wa usimamizi wa raslimali za maji katika kidakio Cha Kikuletwa kilichoandaliwa na Bodi ya maji bonde la Pangani(PBWB) na kufanyika mkoani Kilimanjaro.
Amesema mkoa huo utajiwekea mikakati ya kukabiliana na upungufu wa maji kwani mkoa huo hutegemea maji kutoka vyanzo vya bonde la Pangani ambayo kwa sasa inakabiliwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu huku maji yakipungua.
“Nimearifiwa kuwa Bonde la Pangani ni miongoni mwa mabonde ambayo ukuaji wa idadi ya watu unaenda kwa Kasi zaidi ikilinganishwa na maji yaliyopo ambapo kiasi Cha matumizi ya maji kwa mtu kimefikia mita za ujazo 1,430 kwa wakazi zaidi ya Mil 4” amesema
Aidha mkuu huyo wa mkoa amewataka wadau wa maji na jamii kutoa ushirikiano mzuri katika kudhibiti aina zote za uharibifu wa vyanzo vya maji ili kuepusha uvunjifu wa amani kama mapigano ya wakulima na wafugaji.
Awali akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, mkurugenzi wa bonde Hilo Segule Segule amesema bonde Hilo limeunda jumuiya za watumiamaji ili ziweze kuwasaidia katika udhibiti na utunzaji wa vyanzo hivyo.
Amesema kwa Sasa jumuiya hizo zimekuwa msaada mkubwa katika ngazi mbalimbali ikiwemo kupunguza na kuondoka migogoro katika vyanzo vya maji kwani wamekuwa wasimamizi na wadhibiti wa kwanza katika maeneo Yao.
“Wametusaidia sana katika kupunguza kesi na migogoro isiyokuwa ya lazima maana wakati mwingi wanazuia uharibifu kabla haujatokea lakini pia wamepunguza aina za migogoro tuliyokuwa tunatatua sisi moja kwa moja kwa kutusaidia kuitatua” amesema
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrick Boisafi ametaka mipango kuimarishwa ili jamii ivune maji ya mvua kwa ajili ya kukabiliana pale penye upungufu.
Amesema ni jukumu la wadau kwa pamoja kuhakikisha maji yanayovunwa yanatumika kwa ajili ya umwagiliaji, mifugo na matumizi mengine yatakayoepusha migogoro hususani ya wakulima na wafugaji.
Akiwasilisha mada, afisa mazingira wa PBWB, Eng. Arafa Majidi ametoa wito kwa taasisi za umma kuwa na mipango ya pamoja katika matumizi bora ya ardhi kwani yanahusisha matumizi ya maji.
Amesema idara za mipango miji, kabla ya kuainisha maeneo kwa ajili miradi ya afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara,elimu na mingine kuishirikisha bonde ili lione kama haiathiri vyanzo vya maji.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai akifungua kikao Cha siku mbili Cha kwanza Cha jukwaa la wadau wa usimamizi wa raslimali za maji.
.
Pichani ni mkurugenzi wa Bodi ya maji bonde la Pangani, Segule Segule
Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Patrick Boisafi akitoa neno kwenye kikao hicho
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam