September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali: kila mwanafunzi alale kitanda chake kuimarisha ulinzi wao

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa  Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amekutana na wakuu wa shule za Sekondari nchini huku akiwaagiza walimu wote nchini kuhakikisha katika shule za bweni kila mtoto analala kitanda chake.

Aidha amewataka walimu hao  kufuata muongozo wa malezi, unasihi na ulinzi wa mtoto kwa shule za Msingi, sekondari na vyuo vya ualimu wa mwaka 2020 ,kuangalia na kuyatolea taarifa maeneo yenye changamoto ili kuimarisha ulinzi dhdi ya wanafunzi .

Profesa Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Nchini  (TAHOSSA) ambao amesema miongoni mwa watu wanaotgemewa katika ulinzi na usalama wa mtoto ni walimu.

“Kwa ninyi ni watu muhimu sana hasa katika eneo hili la kumlinda mtoto na maendeleo ya Taifa kwa ujumla hivyo ,mtumie nafasi hii kuanda kizazi chenye tija na weledi.”amesema Prof.Mkenda na kuongeza kuwa

“Tushirikiane kufanya ulinzi wa watoto, hakikisheni shuleni hawalali watoto wawili kitanda kimoja na kama kuna changamoto ya vyoo pia pigeni simu kwa mkurugenzi mueleze changamoto hizo lengo ni kuhakisha mazingira salama ya utoaji elimu na kuwalinda watoto.”

Vile vile amewataka walimu kuangalia maudhui ya vitabu vinavyoingia shuleni ili visiharibu wanafunzi lakini pia kutumia Skauti na Viongozi wa dini katika kuendeleza malezi mazuri ya watoto shuleni.
Kuhusu udanganyifu wa mitihani ,Waziri huyo amekemea tabia hiyo unaofanywa na watumishi wa serikali na sekta binafsi wakiwemo walimu huku akiwataka Wakuu wa shule kutojiingiza katika udanganyifu huona badala yake wasimamie ili usitokee.
Ametoa thadhari kwa wote wenye tabia hiyo ambapo hufungua mitihani na kuwaonyesha watoto kabla ya siku husika ya kufanya mitihani hiyo huku akisema kuwa serikali haitawafumbia macho kwa watakaobainika kufanya hivyo.

 “Mitihani imekuwa ikienda vizuri kwenye Baraza la Mitihani la Tanzania isipokuwa inapokwenda shuleni wamekuwepo watu wachache sana ambao wanajihusisha na udanganyifu na kwamba Serikali haitavumilia udanganyifu huo,”Amesisitiza Prof.Mkenda
Waziri Mkenda amesema kwa sasa kuna kesi zinaendelea kwa wale ambao walituhumiwa kwa kuvujisha mitahani huku akiahidi kuwa hukumu zao zitakopotolewa na mahakama ,majina yao yatawekwa hadharani ili iwe fundisho kwa wengine,”Amesisitiza Prof.Mkenda

Awali Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amewataka wakuu wa Shule kufuatilia utendaji wa walimu shuleni ili kuondoa alama F kwenye masomo wanayofundisha.

“Naendelea kusisitiza kufuatilia utendaji wa walimu, lakini pia wanafunzi wanapoingia shuleni tuanze na kuhakikisha wanakuwa vizuri katika lugha, wanapoilewa na kuiandika inakuwa rahisi kwao kuelewa masomo,”amesisitiza Dkt. Msonde.
Naye  Rais wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Frank Mahenge ameishukuru Serikali kwa namna inavyoshirikiana na Umoja huo na kuiomba pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini kujenga pia nyumba za walimu.