Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na mkakati wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ili kuifanya jamii iepukane na magonjwa hayo pamoja na upatikanaji wa huduma bora za Afya.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na kudhibiti Magonjwa Bi. Valeria Milinga leo Julai 4, 2022 kwenye kongamano la Afya lililohusisha viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka Sekta ya Afya jijini Dar es Salaam.
“Kongamano hili limeandaliwa na wadau wetu wa Christian Social Services Commission (CSSC) ambao wameweza kutualika wadau kutoka sehemu mbalimbali ikijumuisha wadau kutoka Wizara ya Afya wakiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Taifa NHIF wadau wengine kutoka taasisi zisizo za Kiserikali na Asasi za Kiraia”. Amesema Bi. Milinga
Katika kutoa huduma bora, Wizara ya Afya inaendelea na Mpango Mkakati wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza wa miaka mitano (2021 – 2026).
“Kati ya malengo makubwa ni pamoja na uboreshaji wa juhudi mtambuka katika mashirikiano ya kudhibiti Magonjwa haya pamoja na uboreshaji wa huduma za kuzuia magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo utoaji wa elimu ili wananchi waweze kujikinga na magonjwa haya”. Amesema Bi. Milinga
Aidha Bi.Milinga amesema ili kuendeleza kuwa na Afya bora wananchi wanapaswa kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi ya kushughulisha mwili, kuepuka matumizi ya tumbaku ikiwepo sigara, shisha, kupunguza matumizi ya pombe na kuepuka msongo wa mawazo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume ametoa rai kwa watanzania kuzingatia mfumo mzuri wa chakula na kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari.
“Tuzingatie maelekezo na kanuni za Afya ili tuishi vizuri kwa kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuwa magonjwa hayo mengi yanaepukika.” Amesema Dkt. Mfaume
Pia, katika kongamano hilo wamejadiliana namna ya uboreshaji wa huduma za Afya pamoja na takwimu ambapo watafanya tafiti za kuangalia viashiria vya Magonjwa yasiyo ambukiza.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, viongozi kutoka Wizara ya Afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, pamoja na Wadau wa Afya. Washiriki hao wamekubaliana mambo kadhaa ikiwemo, ushirikishwaji wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya viwanda na sekta ya wasafirishaji ili kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza pamoja na Utekelezaji wa Afua ya utoaji wa elimu na uhamasijaji juu ya kujikinga na kudhibiti Magonjwa hayo.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunziÂ
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu