November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imejizatiti kueneza ufundishaji wa lugha ya kiswahili katika nchi za Afrika

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejizatiti kueneza lugha ya Kiswahili kwa kuimarisha ufundishaji wa Kiswahili katika nchi za Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kukabidhi bango la Kiswahili kwa watumishi watakaopanda Mlima Kilimanjaro kwa azma ya kusherehekea Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania kwa kubidhaisha lugha ya Kiswahili Kikanda na Kimataifa, Kaimu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe amesema nia ni kuendeleza Kiswahili kwa kutoa mafunzo kwa watu wengi zaidi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu, Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipa kipaumbele lugha ya Kiswahili kwa kuitangaza ndani na nje ya nchi ikitambua kuwa Uhuru wa Mwafrika upo katika kujikomboa kifikra, kiutashi, kiimani na kutokua na mipaka katika matumizi yake ya lugha ya Taifa.

“Kwa kutambua hilo sisi kama Wizara mama ya mafunzo nchini tunapoadhimisha Uhuru wa Mtanzania Kitaifa tuna fahari kubwa kuipa lugha ya Kiswahili hadhi yake kwa kuipandisha kileleni mwa Mlima Kilimanjaro kwa kauli mbiu “KISWAHILI KILELENI” na kuitangazia Dunia Uhuru wetu, na hamasa yetu ya kujikomboa kupitia lugha hii,” amesema Prof. Mdoe

Aidha amesema kwa sasa lugha ya Kiswahili ina wazungumzaji takriban milioni 250 na kwamba lugha hiyo inafundishwa kwenye Vyuo Vikuu visivyopungua 150 duniani kote.

“Vyuo vya Tanzania vina makubaliano na vyuo vya nje kuendelea kufundisha Kiswahili, hata Wizara ina mikataba takribani minne na Wizara za Elimu za nchi nyingine kuhusiana na masuala ya kufundisha Kiswahili na bado tunaendelea na mazungumzo na nchi nyingine, lengo ni kukikuza Kiswahili,” ameongeza Prof. Mdoe.

Naibu Katibu huyo ametumia muda huo kutoa wito kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuendelea kuchochea matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mataifa hayo ikiwemo kufungua madarasa ya awali ya kufundisha Kiswahili.

“Nchini Malawi tayari tumefungua darasa la kufundisha lugha ya Kiswahili na imewezekana kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini humo ndio maana natoa wito kwa Mabalozi wengine kufanya hivyo ili kuendelea kukuza lugha yetu kimataifa,” amefafanua Prof. Mdoe.

Naye Menna Yasser, aliyekuwa mgeni maalum katika tukio hilo ambaye pia ni mwalimu na mwandishi wa kitabu cha kwanza cha Kiswahili kutoka nchini Misri amesema anajivunia kujua lugha ya Kiswahili na kwamba ni vizuri Waafrika tukahifadhi utambulisho wetu na kujivunia kujua lugha ya Kiswahili.

“Tuongee na kuthamini lugha zetu badala ya kudhani kuzungumza lugha nyingine ndio ustaarabu,” amesema Yasser.

Kwa upande wake Meja Mwinyikombo Ally ambaye ameghani shairi maalum la Kiswahili katika hafla hiyo amesema uhuru, heshima, umoja na utu uliopo baina ya Watanzania umeletwa na lugha ya Kiswahili kwani ndio ilikuwa nyenzo ya kuwaunganisha Watanzania na kupata uhuru hivyo kukiweka Kiswahili juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro ni kuashiria yale aliyokusudia Mwl. Julius Nyerere na jitihada za kuendelea kukibidhaisha Kiswahili.