November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekondari ya Kallaghe yakamilika, kupokea wanafunzi

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

HATIMAYE Shule ya Sekondari Kallaghe iliyopo Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, imeweza kukamilika kwa asilimia 80 na kuweza kupokea watoto 91 wa kidato cha kwanza Januari 9, 2023.

Ni baada ya shule hiyo kuchelewa ujenzi wake kwa miezi tisa kutokana na baadhi ya watu kukataa shule hiyo isijengwe kwenye kata hiyo ya Mgwashi, na kumfanya Diwani wa Kata hiyo ya Mgwashi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Tanga, Sadick Kallaghe kutaka kujiuzulu nyadhifa zote.

Akizungumza Januari 8, 2023 kwenye dua maalumu (maombi) ya kuwaombea watoto watakaosoma shuleni hapo, iliyofanyika kwenye shule hiyo, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava, alisema shule hiyo ilichelewa ujenzi wake kwa miezi tisa kutokana na mvutano uliojitokeza sehemu ilipotakiwa kujengwa shule hiyo.

Mnzava alisema kutokana na Kata ya Mgwashi kutokuwa na shule ya sekondari, waliazimia shule hiyo ambayo ni maalumu, na shule kama hiyo inajengwa moja tu kwenye kila halmashauri kwa Mpango wa SEQUIP kwa fedha kutoka Serikali Kuu, ijengwe Kata ya Mgwashi.

“Kama kuna jambo limenifurahisha ni jambo hili la shule hii kufika mwisho, na hatimaye ujenzi wake kukamilika, na kuanza kupokea watoto kesho (Januari 9). Haikuwa kazi rahisi, sababu fedha za mradi wa shule hii zilikaa kwenye akaunti kwa miezi tisa, tangu Januari, 2022 hadi Septemba 2022 ujenzi ulipoanza.”

“Wito wangu kwenu wananchi wa Mgwashi, mnatakiwa kupeleka watoto wenu shule ili waweze kupata elimu bora, huku mkitoa ushirikiano kwa walimu na uongozi wa shule. Lakini pia, kwa vile ujenzi wa shule bado unaendelea, tunaomba muweze kulinda vifaa vya ujenzi visiibiwe” alisema Mnzava.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini (kichama) Ally Waziri alisema haikuwa kazi rahisi shule hiyo kujengwa Kata ya Mgwashi, na moja ya waliofanikisha shule hiyo ni wananchi kuonesha utayari, na walisaidia mambo mengi kukamilisha ujenzi huo.

“Hii shule tumepambana sana kuona inajengwa hapa. Ilifikia mahali Diwani wa Kata hii (Mgwashi) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga, kutaka kujiuzulu iwapo shule haitajengwa kwenye kata hii, sababu watoto wa kata hii walikuwa wanateseka kwenda umbali mrefu kufuata shule. Nilimueleza usijiuzulu, shule itajengwa” alisema Waziri.

Naye Diwani wa Kata ya Mgwashi Sadick Kallaghe, ambapo kwa heshima, wananchi wameipa shule hiyo jina lake, alisema yeye akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, kata yake ilikuwa ni moja ya kata tatu ambazo hazina sekondari, kati ya kata 29 za halmashauri hiyo.

“Hatujawahi kuanzisha vita tukashindwa. Kama shule isingejengwa ningejiuzulu nafasi zote kuanzia udiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri, na Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga. Kuna watu hawataki maendeleo ya wengi, lakini mimi naelewa watoto hawa wa kata hii walikuwa wanakwenda umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 12 kwenda shule, na kilomita 12 kurudi nyumbani, hivyo shule hii ni mkombozi kwa watoto wa Mgwashi” alisema Kallaghe.

Akisoma taarifa ya shule hiyo kwa mgeni rasmi, Mnzava, Afisa Tarafa ya Bungu Peter Mamuya, alisema shule hiyo inajengwa chini ya Mpango wa SEQUIP.

Shule hiyo iliingiziwa na Serikali Kuu sh. milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, matundu 20 ya vyoo vya wanafunzi, Jengo la Utawala, vyumba vitatu vya maabara, jengo la maktaba na jengo la ICT (Computer Room).

“Mheshimiwa Mbunge, Ujenzi wa Shule ya Sekondari Kallaghe ulianza rasmi Septemba Mosi, 2022, chini ya Usimamizi wa Kamati iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi inayohusisha wajumbe kutoka katika Kata ya Mgwashi pamoja na wajumbe wengine kutoka Shule ya Sekondari Bungu. Mpaka sasa kiasi kilichotumika ni sh. 285,254,600 na kiasi cha fedha kilichobaki ambacho bado hakijatumika ni sh. 184,745,400” alisema Mamuya.

Mamuya alisema shule hiyo ambayo itakuwa ya bweni na kutwa, huku bweni la wasichana likijengwa na mfadhili, vyumba vya madarasa yote manane yamekamilika na yapo tayari kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi 91 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023. Jengo la ICT nalo lipo katika hatua ya umaliziaji, mafundi wanaweka PVC board pamoja na kufanya scheming kwenye kuta za ndani za jengo.

Ujenzi wa vyoo nao upo katika hatua ya umaliziaji.

Mafundi wanakamilisha hatua ya ujenzi wa chemba, kuweka milango katika vyumba vya vyoo, kupiga chuping na kufanya scheming.

Ujenzi wa jengo la utawala upo katika hatua ya Lenta.

Mafundi tayari wameshamwaga zege kwenye box la lenta ambapo wanategemea kuanza kujenga kozi mbili za mwisho.

Majengo ya maabara yanahusisha maabara zote tatu zikihusisha bailojia, kemia na fizikia. Maabara zote zipo katika hatua za ujenzi wa Lenta.Mafundi wanatarajia kujenga kozi mbili za mwisho. Ujenzi wa jengo la maktaba upo katika hatua za ujenzi wa Boma.

Mafundi wanatarajia kukamilisha Boma ndani ya siku mbili zijazo.

“Ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalaghe unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni kuongezeka kwa gharama ya vifaa vya ujenzi, mabadiliko ya hali ya hewa hususani katika kipindi cha mvua inakuwa ni ngumu kusafirisha vifaa vya ujenzi kutoka Korogwe kuja Mgwashi.Mazingira magumu ya kupata gari za kusafirishia vifaa vya ujenzi.”

Hii inatokana na ubovu wa miundombinu hususani barabara ambapo wamiliki wa magari wanahofia kuharibika kwa magari yao.

“Pia tunatarajia kwamba mradi huu utakamilika rasmi kwa kuyakamilisha majengo yote yaliyobaki Januari 30, 2023. Tukumbuke kwamba hadi sasa majengo yote ya madarasa nane, Jengo la ICT na vyoo vya wanafunzi yamekamilika ujenzi wake. Isipokuwa kwa Jengo la Utawala, maabara zote tatu na jengo la maktaba, ambapo kwa jitahida na mikakati tunayoipanga tunadhamiria kuwa majengo yote yaliyobaki yatakamilika mwishoni mwa mwezi wa kwanza” alisema Mamuya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Twalib Mzenga, alisema fedha za mradi huo ni za mwaka wa fedha 2021/2022, na mgogoro uliochelewesha ujenzi wa shule hiyo, ni baadhi ya wananchi kudai eneo inapotaka kujengwa shule hiyo ni kwao, hivyo wanahitaji fidia.

Hata hivyo mmiliki wa Kiwanda cha Chai Dindira (MeTL) alisema eneo hilo ni lake, na anatoa bure kwa wananchi wajenge shule.

Hata hivyo, mwisho wa siku, Serikali ilitoa fidia kwa watu hao, na shule ikajengwa.

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga Timotheo Mnzava akizungumza kwenye dua (maombi) ya ufunguzi wa Shule ya Sekondari Kallaghe iliyopo Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Ally Waziri akizungumza kwenye dua (maombi) ya ufunguzi wa Shule ya Sekondari Kallaghe iliyopo Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bungu, ambaye pia ni refarii wa Ligi Kuu ya Tanzania Mohamed Mkono, akizungumza kwenye dua (maombi) ya ufunguzi wa Shule ya Sekondari Kallaghe iliyopo Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. Mkono ndiyo alikuwa Msimamizi wa Shule mpya ya Sekondari Kallaghe. (Picha na Yusuph Mussa).
Madarasa ya Shule ya Sekondari Kallaghe iliyopo Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Wananchi waliohudhuria dua (maombi) Shule ya Sekondari Kallaghe iliyopo Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).