
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga Husna Sekiboko ameiomba Serikali kuwa na Mpango madhubuti utakaowezesha vijana wanahitimu masomo ya Ufundi wanakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kile walichojifumza na hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira nchini.
Sekiboko ameyasema hayo Leo Aprili 16 mwaka huu Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambayo imeomba kuidhinishiwa zaidi ya shilingi Trilioni 11 katika mwaka wa Fedha wa 2025/2026.
Amesema ,Serikali kwa dhamira yake njema imeshajenga shule za Ufundi 100 nchini kwa maana ya mkondo wa Amali kwa lengo la kutoa Elimu ya Ufundi lakini hakuna miundombinu ya kuwezesha ufundishaji kwa vitendo .
“Shule zimejengwa lakini ziko wapi karakana,wako wapi walimu wa Ufundi ,viko wapi vifaa vya Ufundi vitakavyokidhi Elimu ya Ufundi tunayoihitaji,
“Tumeshakuwa na Elimu ya Ufundi kwa kipindi kirefu lakini tuepuke kwenda kwa mazoea ,tumeshafindisha watoto wetu kwa nadharia kwa kipindi kirefu ,Elimu ya Ufundi tunayoitamani ni ya watoto kupewa ujuzi ili watoke shuleni akiwa na uwezo wa kujiajiri na kufanya kazi kwa ufanisi ,
“Kwa hiyo tungependa kuona shule zinazojengwa kwa ajili ya wanafunzi wa Amali ,VETA kunakuwa na walimu wa kutosha na wenye ujuzi ili tudhamirie kwa pamoja Kutoka tulipo kwenda hatua nyingine na kutuletea ule uzalishaji na kupanua soko la ajira nchini.”amesema Sekiboko na kuongeza kuwa
“Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara mkoa wa Tanga wiki mzima,lakini maono yake katika maelezo aliyotoa alitamani kurejesha Tanga ya Viwanda ambayo haiwezi kupatikana bila malighafi,ni lazima tuwaandae vijana kuzalisha malighafi kwa ajili ya Viwanda ambavyo vinadhamiriwa lakini pia tuwaandae vijana kuajiriwa kwenye viwanda.”amesema
Aidha amesema kuwa hayo yote yanahitaji uwekezaji katika Elimu ya Ufundi ambayo ni gharama zaidi.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo,kwa shule za Ufundi zilizopo nchini hivi sasa ,zinahitajika shilingi bilioni 135.5 ili ziweze kupata vifaa huku akisema walimu wa kufundisha Ufundi waliopo ni 1,000 ambao ni nusu tu ya walimu zaidi ya 2,000 wanaohitajika.
“Sasa kama tuna dhamira ya dhati ya kwenda kwenye Elimu ya kujitegemea itakayoleta manufaa kwa watanzania ni lazima tujikite katika Elimu ya Ufundi yenye tija kwa kupeleka vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule ambazo tumeziandaa .”amesisitiza Sekiboko
More Stories
Chalamila:Dar ni salama,aelezea mafanikio na mipango ya maendeleo ya Mkoa
Ulaji vyakula vya aina moja,umri vyatajwa ongozeko la matatizo ya macho Mbeya
Kenya,Uganda zaanzisha mradi wa uendelezaji rasilimali za maji Angololo