November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SCAN CODE, SIDO wasaini MOU kuwainua wafanyabiashara

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KAMPUNI ya SCAN CODE kwa kushirikiana na shirika la kuendeleza viwanda Vidogo nchini Tanzania (SIDO) wamesaini MOU ya muda wa miaka mitatu lengo ni kuwasaidia wajasiriamali ili waweze kufanya biashara kidigitali na Hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 6, 2024 katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya kimataifa Sabasaba Jijini Dar es Salaam, Mwekezaji na Mkurugenzi wa Kampuni ya Scan Code, Mgimba Faustine amesema pia lengo lao ni kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupambana na bidhaa bandia katika soko la Tanzania.

“Mpaka kufikia miaka mitatu tutakua tumeongeza tija zaidi sana katkka soko letu na wajasiriamali wengi watakua wamefaidika na huduma za scan code ambapo watakuwa wamepata QR Code kwa wingi na Bar code zinazosaidia uuzaji wa bidhaa kwenye soko” amesema

Aidha amesema mpaka sasa wamewafikia wajasiriamali wengi kwani wako nchi nzima ambapo kila Mkoa wameweza kupata wajasiriamali takribani 20

Pia amesema wameingia makubaliano na Shirika la Viwango (TBS) lengo ikiwa ni kuwafikia wazalishaji wakubwa ambao pengine wasingeweza kuwapata kupitia SIDO.

Mgimba aliwataka watanzania wote kutembelea banda lao ili kupata huduma na Elimu mbalimbali ikiwemo kujua uwezo wa QR Code, uwezo wa TEHAMA na Bar code

“Tunawaalika wadau wote kufika katika Banda la SIDO na Scan code ili kupata huduma na Elimu mbalimbali kujua uwezo wa QR Code, uwezo wa TEHAMA, Bar code na thamani yake katika bidhaa mbalimbali kwenye soko letu la Kitanzania”

Kwa upande wake Meneja masoko kutoka shirika la kuhudumia viwanda Vidogo ( SIDO)- Lilian Massawe amewataka wajasiriamali wazidi kujiunga SIDO ili waweze kuunganishwa na taasisi zingine ikiwemo SCAN CODE TANZANIA ambao amewawezesha wajasiriamali kwa gharama nafuu.

“Nawahimiza watumie huduma hii ya misimbo milia pamoja na Scan code ili waweze kufanya biashara kidigitali, ili uweze kuingia kwenye masoko mbalimbali ya kimataifa lazima ufanye kazi zako kidigitali na hivyo kuweza kuwafikia wateja wengi “amesema Lilian.