December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SBL yakabidhi mradi wa maji Magu

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda (Katikati), Mkuu wa Wilaya ya Magu Joshua Nassari (Kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Obinna Anyalebechi (Kushoto) wakiwa mbele ya moja kati ya vituo 13 vya usambazaji wa maji kijijini hapo.

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Bia Serengeti na shirika lisilo la kiserikali, African Community Advancement Initiative (AFRIcai) wamezindua mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 215 katika Kijiji cha Kabila wilayani Magu mkoani Mwanza ikiwa ni jitihada za kuwapelekea maji safi na salama wananchi wa eneo hilo.

Ukiwa na uwezo kwa kuhudumia wakazi 12,000 mradi huo unahusisha ufungaji wa pampu ya kuzamisha ndani ya kisima, ujenzi wa nyumba ya pampu, tanki la kuhifadhi maji, mtandao wa mabomba ya maji, na vituo vipya vya maji 13 vyenye uwezo wa kutoa mita za ujazo 87,000 za maji kwa mwaka.

katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwapongeza SBL na AFRIcai kwa kutoa msaada muhimu kwa wakazi wa Kijiji cha Kabila, alinukuliwa, ‘‘mashirika haya binafsi yamekuwa mstari wa mbele katika kukuza miradi ya maendeleo nchini ambayo inawezesha kuwepo kwa jamii iliyo na uzalishaji na afya bora. Mtanda aliongeza, ‘‘Ushirikiano kati ya SBL na AFRIcai unathibitisha dhamira ya sekta binafsi kwa uwajibikaji wa kijamii na maendeleo endelevu. Kwa kuwekeza katika miradi inayolenga mahitaji msingi ya jamii kama usambazaji wa maji, SBL na AFRIcai wanadhihirisha dhamira yao ya kuboresha ustawi wa jamii ya watanzania na kuchochea mafanikio ya muda mrefu.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi alisema kuwa mradi huo ambao unajulikana, Water for Life (Maji kwa ajili ya uhai) ni miongoni mwa mikakati ambayo kampuni hiyo ya bia inaendesha katika mikoa ya Iringa, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mwanza, Singida, Mara, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma ikiwa imewanufaisha zaidi ya watu milioni mbili kwa maji safi na salama.

“Mwaka huu, Serengeti Breweries Limited (SBL), kwa kushirikiana na African Community Advancement Initiative (AFRIcai), tumekamilisha ujenzi wa mradi huu muhimu wa maji katika kata ya Kabila, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza. Kwa kutambua kwamba maji ni hitaji la msingi la maisha na moja ya rasilimali muhimu zaidi, SBL kupitia mpango wake wa kusaidia jamii, imekuwa ikitekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kutoa maji bure kwa watu wanaoishi katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji nchini. Kupitia sera ya Water fo Life hadi sasa tumetekeleza miradi 26 ya maji katika maeneo yenye uhaba wa maji katika sehemu mbalimbali za nchi, ambapo zaidi ya watu milioni 2 wamenufaika na miradi hii ambayo inalenga kutoa maji safi na salama.”

Nae Meneja wa Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu alisema, “Mradi wa Kabila sio tu kwamba utaboresha afya za wakazi wa eneo hilo bali pia utaongeza tija kiuchumi hususani kwa watoto wa kike na wanawake ambao hawatahitaji kutumia saa nyingi kutafuta maji safi na salama sehemu nyingine. Hii inawapa fursa ya kuhudhuria shule wakiwa huru.”

Akihutubia katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la African Community Advancement Initiative (AFRIcai) Bonus Caesar aliongezea kwa kusema kuwa shirika hilo lina sera zilizojikita katika ustawi wa jamii katika maeneo ya maji, afya, elimu na uwezeshaji.

Caesar alisema “Ushirikiano huu wa kimkakati baina ya SBL na AFRIcai unalenga kuondoa uhaba wa maji kwa kuwapatia maji safi na salama wananchi 11,927 katika vitongoji vya Ilambu, Mlimani, Igogo, Shuleni na Majengo”