December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAUT-yamuenzi Mwl Nyerere kwa kutembelea nyumbani kwake Mwitongo Butiama

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Butiama

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostine(SAUT) Mkoa wa Mwanza wametembelea nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,kwa ajili ya kufahamu na kujifunza historia ya maisha yake.

Hii ikiwa njia moja wapo ya kumuenzi Mwalimu Nyerere na kufanya vijana nchini kufahamu historia ya maisha yake kwani wengi wa vijana hawaifahamu.

Ziara hiyo iliofanyika Oktoba 13,2022 ambayo iliongozwa na Makamu Mkuu wa chuo cha SAUT Profesa Costa Mahalu,akiwa ameambatana na watendaji wa chuo hicho, viongozi wa dini pamoja na wengineo.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo Makamu Mkuu wa chuo cha SAUT Profesa Costa Mahalu,ni kumuenzi baba wa Taifa huku akieleza kuwa mara nyingi akiwafundisha wanafunzi wake wa uzamili inaniuma sana akiwauliza juu ya Mwalimu Nyerere ni nani hawamfahamu,hivyo ni kitu ambacho kinaniumiza kweli.

Profesa Mahalu,ameeleza kuwa kutokana na vijana kutofahamu historia ya Mwalimu Nyerere basi sifa,fikra na falsafa zake zinaweza kupoteza.

“Sisi pale chuoni tukasema hapana Mwalimu ndio sisi,ndio taifa letu,ndio alituletea Uhuru,kwanini leo hii vijana wetu wamsahau,tumekuja huku kusikiliza na kumfahamu Mwalimu lakini ukienda nchi nyingine wanamuenzi wanajua ni nani,lakini kwanini sisi vijana wetu hawamjui,”alihoji Profesa Mahalu.

Hivyo tumeona ni vyema kabla ya kongamano la Mwalimu Nyerere Oktoba 14 vijana wetu waje kutembelea nyumbani kwake,wajifunze historia yake, falsafa zake,fikra zake,kuona amelala wapi.

“Tuendelee kumkumbuka katika maisha yetu na kutenda yale alioyatenda tumesikia alikuwa muadilifu, kiongozi ambaye alipenda watu basi nasi tupende watu tuheshimu watu katika maisha yetu ya uongozi na Mwalimu awe taa yetu,”ameeleza Profesa Mahalu.

Baada ya kupokea ugeni huo mtoto wa Baba wa Taifa,Madaraka Nyerere ameeleza kuwa vijana wengi hawamfahamu Mwalimu Nyerere,hivyo ametoa ombi kwa vijana kusoma historia ili wamfahamu vizuri Mwalimu Nyerere kuwa alikuwa anajaribu kufanya nini.

“Suala ni kumuenzi lakini siyo kila kitu alifanya ni kizuri lakini kuna mambo baadhi aliyofanya ambayo tunaweza kuendelea nayo mpaka leo hii,yale machache mlijifunza kuhusu Mwalimu Nyerere mkawasimulie na wengine ili wapate shauku ya kuweza kuja kutembelea na kufahamu alikuwa ni mtu wa namna gani,alikuwa na falsafa zipi,”ameeleza Madaraka.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma- SAUT Prof.Hossea Rwegoshora, ameeleza kuwa watayaenzi yale mema aliyofanya Mwalimu Nyerere.

“Kumuenzi Mwalimu Nyerere ni kuchukua yale mema na kuyaishi,tubadilike tusimuenzi kwa mdomo,kwa maneno na makongamano iwe kwa matendo yetu na imani zetu viendane na yale aliofanya na tumejifunza mengi,”ameeleza Prof Hossea.

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini,ameeleza kuwa kupitia ziara hiyo kama Kamati ya amani wameguswa na wamejufunza uwepo wa Mungu,kutosheka pamoja na kutenga muda wa kuzungumza na watoto.

“Kilichopo nchi sasa ni mmomonyoko wa maadili,malezi yamepotea wazazi hawana muda wa kukaa na watoto lakini ninyi ni mashaihidi,tumeshuhudia picha za watoto wa Mwalimu akiwa na familia yake na muongozaji ametuonesha viti alivyokuwa akikalia Mwalimu mke wake pamoja na watoto wake, tumejifunza kuwa Mwalimu alikuwa na muda wa kuongea na watoto wake na familia,leo wapo watu wameoa na kuolewa ila hawana nafasi ya kuzungumza na watoto wala familia yake,”ameeleza Sheikh Kabeke.

Makamu Mkuu wa chuo cha SAUT Profesa Costa Mahalu(kushoto) akizungumza na mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,Madaraka Nyerere,wakati chuo hicho kilipofanya ziara ya kutembelea nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwitongo Butiama kwa ajili ya kumuenzi na kufahamu historia ya maisha ya Mwalimu Nyerere.(Picha na Judith Ferdinand)
Mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,Madaraka Nyerere,akizungumza mara baada ya kupokea ugeni kutoka chuo cha SAUT kilipofanya ziara ya kutembelea nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwitongo Butiama kwa ajili ya kumuenzi na kufahamu historia ya maisha ya Mwalimu Nyerere.(Picha na Judith Ferdinand).
Makamu Mkuu wa chuo cha SAUT Profesa Costa Mahalu(mwenyewe tai nyekundu),akiwa na viongozi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza na msafara mzima wakisikiliza maelekezo kutoka kwa muongozaji anayeelezea historia ya Mwalimu Nyerere wakati chuo hicho kilipofanya ziara ya kutembelea nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwitongo Butiama kwa ajili ya kumuenzi na kufahamu historia ya maisha ya Mwalimu Nyerere.(Picha na Judith Ferdinand)
Makamu Mkuu wa chuo cha SAUT Profesa Costa Mahalu(mwenyewe tai nyekundu),akiwa na viongozi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza na msafara mzima wakifanya sala katika kaburi la Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, wakati chuo hicho kilipofanya ziara ya kutembelea nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwitongo Butiama kwa ajili ya kumuenzi na kufahamu historia ya maisha ya Mwalimu Nyerere.(Picha na Judith Ferdinand)