January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia uso kwa uso na vigogo wa Taasisi na Mashirika ya Umma

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali

Akizungumza katika kikao na wahariri na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema kikao hicho kitafanyika Agosti, 2024 katika Ktuo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Kikao hicho kitakuwa na kauli mbiu isemayo;

” ‘Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma Kuwekeza Nje ya Tanzania’ ambayo inalenga kuhimiza Taasisi na mashirika ya umma kuangalia zaidi fursa za kuwekeza au kupanua wigo wa huduma nje ya Tanzania. “

Pia amesema kauli mbiu hiyo inaunga mkono maelekezo ya RAIS Samia, aliyoyatoa wakati wa Kikao Kazi cha mwaka jana ( 2023) ambapo katika kikao hicho alielekeza kuangalia uwezekano wa Taasisi na Mashirika kufanya biashara au kupelekea huduma zake nje ya Tanzania.

Mchechu ameyataja maeneo muhimu yatakayofanyiwa kazi katika kikao kazi hicho cha pili.

“Kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika kikao kazi cha mwaka 2023,

Mbili, kujadili fursa za kikanda na kimataifa kwa ajili ya Taasisi na mashirika kuwekeza nje ya nchi; Kujadili na kupata uzoefu wa kiutendaji kutoka kwa wataalam wa ndani na nje ya nchi waliofanikiwa kiutendaji tukiangazia nchi za Singapore, China, UAE na S.Africa”, alisema na kuongeza;

“Namna bora ya kuboresha mitaji ya Mashirika yetu ili kuleta ufanisi wa kiutendaji na kuongeza ushindani, Kubadilisha mitazamo na kuzifanya Taasisi na Mashirika yetu kuwa vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi na
tutapitia kwa pamoja na kukumbushana kuhusu mambo mengine muhimu ambayo Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wanapaswa kuzingatia katika usimamizi wa utendaji kazi ikiwemo miongozo mbalimbali ya Uendeshaji wa mashirika ya umma pamoja na umuhimu wake katika kutekeleza malengo ya Serikali kwa ufanisi”.

Pia amesema watajadili changamoto mbalimbali za kiuendeshaji katika Taasisi pamoja na kuainisha mikakati ya kukabiliana nazo; na vilevile Taasisi zilizofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utendaji kazi kama vile kutengeneza faida na kufanya mageuzi ya utendaji na hivyo kuboresha utoaji wa huduma zitatambuliwa na kupewa tuzo.

Kuhusu Matokeo ambayo yanatarajiwa
baada ya kikao kazi hicho, mchechu amesema ni Taasisi kujielekeza katika uwekezaji wa nje ya nchi; kuona Taasisi zikiendeshwa kwa ufanisi, zile zinazofanya biashara zitaongeza faida na hivyo kutoa gawio kwa mujibu wa sheria; Kwa taasisi ambazo zilianzishwa kwa misingi ya kutoa huduma zitaongeza uwezo wa
kujitegemea katika uendeshaji wake; na kuendelea kuwepo kwa mfumo endelevu ya kuzitambua taasisi zinazofanya vizuri na kuchukua hatua stahiki kwa taasisi ambazo hazifanyi vizuri .