*Asema alikuwa mtulivu kwa mamlaka za uteuzi, kila alipopelekwa aliacha alama
Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema yeye pamoja na vijana wa leo wanatakiwa kujifunza kutoka kwa Hayati Edward Sokoine, uadilifu, uaminifu na uchapa kazi wake na kwamba sifa ambazo anapenda kuzisisitiza kwa viongozi wa sasa na wajao.
Rais Samia alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Edward Moringe Sokoine cha Maisha na Uongozi Wake.
Alizidi kufafanua kwamba Sokoine alikuwa mwaminifu sana kwa mamlaka yake ya uteuzi na kwa wananchi, ndiyo maana haishangazi kwamba alikidhi majukumu mengi na makubwa katika umri mdogo.
“Katika hili tunajifunza kwamba ukiwa mwaminifu na mchapakazi hauhitaji kukimbizana na vyeo, bali vyeo vinakuja vyenywe, vinakufuata pale ulipo,” alisema Rais Samia.
Alitaja funzo jingine wanalojifunza kutoka kwa Hayati Sokoine kuwa ni uongozi unaoacha alama. “Alama alizoacha Sokoine ziko karibu kila sekta alizopita, ambapo akiwa Waziri Ndogo wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alisimamia ujenzi wa Reli ya TAZARA ambayo hivi karibuni nilipokuwa Beijing, China yeye na wenzetu wa Zambia wameamua kukarabati reli hiyo na kuifanya ya kisasa.
Reli hii ilikuwa na mchango mkubwa katika vita ya ukombozi Kusini mwa Afrika na ni dhamira yetu kuifufua ili itusaidie katika kutimiza malengo ya umoja wa Afrika ili kufikia lengo la nchi za Afrika kufanya biashara kwa wepesi.
Alitaja alama nyingine ambayo wanaiona, Rais Samia alisema ni pale alipokuwa waziri wa Ulinzi na JKT ambapo alishauri na ikaridhiwa wanawake waanze kuandikishwa jeshini.
“Hii isingetegemewa kutoka kwa wamasai ambao wamekulia kwenye jamii ya Wamasai ambapo wakati ule nafasi ya mwanamke ilikuwa chini kabisa.
Lakini, Sokoine hakutaka mila potofu ziharibu ndoto zao, badala yake alipambana na wanawake wakaanza kuandikishwa jeshini, leo hii tunaona hadi majenerali wanawake na vyeo vyao havipatikani kwa sababu wao ni wanawake , bali kwa uwezo wao,” alisema Rais Samia na kuongeza kwamba kwenye kilimo Sokoine aliamini katika kilimo cha kisasa kwa kutumia wataalam wenye stadi stahiki, hivyo alisimamia uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) ambacho kilikuja kupewa jina lake.
“Leo hii SUA inaendelea kuishi maono ya Sokoine ya kuzalisha wataalam wengi wanaoendeleza sekta ya kilimo na mifugo.”
Alitaja somo jingine kutoka kwa Sokoine ni uwezo wa kutafuta majibu ya changamoto kwa kutumia raslimali zilizopo ndani. Alitoa mfano kuwa wakati Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilipokuwa na upungufu wa mabasi na hivyo kuathiri usafiri wa abiria, Sokoine alielekeza kuwa mabasi ya mashirika ya umma baada ya kuwafikisha watumishi majumbani kwao, mabasi hayo yatumike na UDA kwa kipindi ambacho mashirika hayo hayayatumii.
Aliongeza kwamba ubunifu huo wa kiuongozi unamkumbusha pia simulizi kwenye Kitabu cha Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, kuhusu pendekezo la Hayati Sokoine lililozua gumzo ndani ya Tanzania, pale alipopendekeza usafiri wa kutumia punda kwa maofisa waliopo vijijini.
“Na hiyo ni kwa sababu kule Umasaini wanatumia Punda , kwa hiyo asingeweza kupendekeza baiskeli, labda angekuwa ametoka kanda ya ziwa. Hata hivyo pendekezo hilo halikutekelezwa, lakini tunaona dhamira yake kiuongozi katika kutafuta majibu ya dhiki za wananchi.”
Aidha, Rais Samia alisema Sokoine alisimama imara katika kipindi ambacho nchi ilikubwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi, miundombinu, uhaba wa chakula na changamoto katika sekta za viwanda na afya.
“Aliweka mkazo kuendeleza kilimo, kufanya mageuzi katika uchumi kwa kuruhusu uchumi huria ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuboresha huduma,” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliongeza kwamba mafunzo ya kiuongozi kutoka kwa Sokoine yanaonekana pia wakati wa chokochoko za Nduli Idd Amin alipovuka mpaka na kukalia sehemu ya ardhi yetu.
“Sokoine alitimiza wajibu wake kikamilifu sio tu Amin kuondoka katika ardhi yetu, bali pia alikimbia nchi yake ,” alisema Rais Samia na kuongeza;
“Vile vile Sokoine aliongoza vita dhidi ya uhujumu uchumi, japo alifariki kabla ya kuona matokeo yake, lakini dhamira yake ilikuwa wazi.”
Alisema funzo kubwa zaidi kutoka kwa Sokoine ni uadilifu, uaminifu na uchapaji kazi. Alisema kitabu hicho kinatupa nafasi ya kujitathmini hali tuliyokuwa nayo miaka 40 iliyopita na hali tuliyonayo hivi sasa.
Alisema hatujafika kule tunakotaka kwenda lakini si haba, bidhaa ambazo tuliziona wakati ule wewe ni uhujumu uchumi, sasa ni bidhaa za kawaida kwenye maduka yetu.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa