January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia: Sina kundi ninapofanya teuzi

Na Penina Malundo,TimesMajiraOnline,Dar

RAIS wa Samia Suluhu Hassan, amesema yeye hana kundi lolote pindi anapofanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, bali anachoangalia ni utendaji wa kazi.

Rais Samia aetoa kauli jana Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuapisha wakuu wa mikoa aliowateua.

Sina kundi, mimi ni mama wa Watanzania wote anayefanyakazi vizuri ni wangu, hata wanaofanya kazi vibaya ni wangu pia,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Mwanzo nilipoanza kuwaapisha wakuu wa mikoa niliwaambia kuwa mlitegemea ningewachagua kwa makundi, lakini niliwaambia mimi kama Samia sina kundi na mkijitazama humo, hayo makundi mnaoyajua wote mpo humo?”

Alisema anayefanyakazi vizuri atampa zawadi, anayefanya vibaya atamchapa mikwaju na wapo anaowachapa na kuwakeka nje kidogo, wakishakuwa kimaadili anamwambia sasa njoo tufanye kazi.

Alisema kwake yeye ni kazi, na anataka viongozi kufanya kazi ili kuivusha nchi hii.

***Siri ya mabadiliko ya viongozi  

Alisema mabadiliko ya viongozi yanayofanyika yanatokana na tathmini ya utendaji inayofanywa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)

Aliongeza kuwa TAMISEMI imekuwa ikifanya tathmini hiyo kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala na pale kunapoonekana kuna shida, hatua huchukuliwa.

Samia alisema wakati mwingine mtu hafanyi vizuri kwa yeye mwenyewe alivyo na wakati mwingine ni mazingira yaliyopo katika eneo, mambo ambayo kwa pamoja huzingatiwa.

Alisema kupitia tathmini hiyo imemfanya, Paul Chacha, kuonekana amefanya vizuri ndiyo maana amepandishwa kuwa mkuu wa mkoa kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua.

***Ataja sababu za kumbadilisha RC Serukamba

Rais Samia alitaja sababu ya kumbadilisha kituo cha kazi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akisema ni kutokuelewana na baadhi ya viongozi wa eneo hilo na kusababisha ‘vimaneno maneno. Serukamba ameapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Maelekezo kwa wakuu wa mikoa

Aidha, Rais Samia alitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa, ambapo alimtaka Lutenali Kanali Patrick Sawala, ambaye amepandishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kutokana na kazi nzuri aliyofanya alipokuwa mkuu wa wilaya, kufanya vyema zaidi, kwani anamwamini  atawakilisha vyema.

Kutokana na Mkoa wa Mtwara kupakana na Msumbuji alimtaka kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama na kamati ya ujirani mwema kufanya vikao na kukubaliana kuondoa changamoto hasa za mpakani.

“Pia katumie Kamati hizo kukuza biashara baina yetu, kumekuwa na malalamiko kuwa tumeanza kufungua eneo zinapita biashara, mkianza kusimamia usalama na biashara ikikua, tuna mengi ya kuuza Msumbuji kuliko wao kuleta kwetu,” alisema Samia.

Alisema mkoa huo pia ni muhimu kiuchumi kutokana na zao la korosho, hivyo alimtaka kusimamia jitihada za Serikali kuongeza uzalishaji wa korosho, kwani aliyeondoka amefanya vizuri licha ya kuwapo changamoto ndogo ndogo.

“Mbali na uongezwaji wa thamani wa zao la korosho, usafirishaji pia, tumeamua korosho yote isafirishwe kutoka Bandari ya Mtwara tumejaribu msimu uliopita na mpaka leo hatujapata lawama kutoka duniani kuwa korosho iliyopelekwa ni chafu,”alisema.

Alisema korosho inaporuhusiwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, mambo mengi yamekuwa yakifanyika katikati.

Pia alisema Serikali imeanzisha kongani ya viwanda vya kubangua korosho mkoani humo, huku akimtaka mkuu huyo wa mkoa kusimamia vyema ili vijana wapate kazi.

Katika mazao ya mbaazi na ufuta alisema Serikali imepata soko lake nchini India na mwaka jana bei ilikuwa nzuri, huku akieleza kuwa bei hiyo inaweza kufanya watu wengi kuzalisha zaidi.

Alimtaka mkuu huyo mpya wa mkoa, wakati wa manunuzi ya ufuta na mbaazi asimamie vizuri, kwani Serikali imeamua mazao hayo yaingie ghalani licha ya kuwa yanauzwa kwa nchi moja, lakini ina wanunuzi tofauti ambao lazima washindane ili Watanzania wapate bei kubwa.

“Pia Mtwara kuna fursa za kitalii ambazo bado hazijatumika, unaweza kwenda kuwa na timu za kitaalamu kuangalia fursa zilizopo, kuziibua na kufanyiwa kazi, zamani Mtwara na Lindi ilikuwa inaitwa mikoa ya pembezoni, mikoa masikini, lakini ni mikoa yenye rasilimali kubwa hivyo nenda kasimamie,” alisema Samia.

***Mkoa wa Songwe

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Samia alisema wamempeleka Daniel Chongolo, kwa sababu anaijua vizuri tangu akiwa ndani ya chama.

Alisema ana imani kuwa amempatia mkoa anaoufahamu na atausimamia vizuri. Alisema mkoa huo unaunganisha Tanzania na Zambia, kupitia Tunduma, huku akieleza kuwa eneo hilo lina mambo mengi ya kiuchumi yanatokea ikiwemo uhalifu mwingi wa kiuchumi.

“Una mkurugenzi mzuri kidogo, ameweza kuongeza mapato, nenda kasaidiane naye, mfanye kazi vizuri pale Tunduma panaweza kuendesha mkoa na mkachangia vizuri Serikalini,” alisema .

***Shinyanga

Rais Samia alisema uzoefu wa kiuongozi alionao  Annamringi Macha, miongoni mwa sababu za yeye kupewa cheo hicho, kwani ana uzoefu.

Samia alimtaka Macha kusimamia kuongeza uzalishaji pamba, kupandisha hali za wananchi kujiletea maendeleo, kwani kumekuwa na hali ya watu kulala na kufuatilia kwa karibu kongani ya Buzwagi inayotarajia kuanzishwa, huku akimtaka kuisimamia kwa ukaribu ili ufanikiwe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya Uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Machi, 2024.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya Uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Machi, 2024.
Viongozi mbalimbali (Wakuu wa Mikoa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano na Mazingira),Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka (UDART) wakila Kiapo cha Maadili kwa viongozi wa Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Machi, 2024.