December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia atoa maelekezo kwa Jafo, Bashe uzalishaji wa sukari

Na Jackline Martin

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Waziri wa Viwanda, Suleiman Jafo kuangalia namna ya kuziweka sera za nchi ili viwanda viweze
kuzalisha sukari, lakini pia wazalishaji kuzalisha ethanol kwa ajili ya kupata nishati safi ya kupikia na kwa matumizi mengine.

Rais Samia alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki Jijini Morogoro wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero K4 na kuweka jiwe la msingi upanuzi wa Mtibwa na Mkulaz,i ambapo alisema kutanuka kwa kiwanda hicho kunailetea nchi mambo mengi ikiwemo uzalishaji utakwenda kuhifadhi fedha za kigeni.

Pia alisema kinaipa nchi uhakika wa kuwa na sukari ndani ya nchi na chakula “Katika mahitaji yetu ya sukari nchini nimeambiwa tani 650,000 ni matumizi ya sukari tunayotumia majumbami, lakini viwanda vinahitaji tani laki 250,000, hizo tukiendelea kuagiza ni upotevu wa fedha za kigeni,” alisema

“Twendeni tukavipe kazi viwanda vyetu kwani vinaweza vikatuzalishia sukari ya viwandani,” alisema Rais Samia

Aidha Rais Samia alimuagiza Waziri Bashe kukaa na wazalishaji wa sukari wa kiwandani kujadiliana changamoto zote kwa upana na kuona namna ya kwenda kuzitatua ili uzalishaji wa sukari nchini usiwe na usumbufu.

Rais Samia alisema Serikali inatambua umuhimu wa viwanda vya sukari nchini na inatamani viimarike, viongeze tija na uzalishaji ili viweze kunufaika na soko la ndani na nje

“Katika kufungua soko la nje Serikali inaweka Miundombinu ya uhakika ya usafiri na usafirishaji uwepo wa SGR inayofika Dodoma lakini baadaye 2028 tutafika Kigoma tutaunganisha na DRC huko ni kufungua soko”

Mbali na hayo, Rais Samia alisema Serikali imekua ikiunga mkono viwanda vya sukari ikiwemo kutoa msamaha wa kodi ambapo kodi iliyosamehewa katika viwanda vitano nchini ni jumla ya sh. bilioni 246 huku kiwanda cha Kirombero kikiwa kimesamehewa kodi ya sh. bilioni 29.

Kadhalika, Rais Samia alisema Serikali inaamini katika sekta binafsi ndiyo maana inaendelea kuimarisha sera na sheria mbalimbali ili kuimarisha mazingira ya biashara nchini, hivyo aliahidi kuendelea kufanya hivyo kwa kufanya mashauriano na majadiliano ambapo pale watakapokamilisha watakuwa tayari kubadilisha sera na sheria za nchi ili biashara zifanyike kwa raha ndani ya nchi

“Lengo ni kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa chakula. Nawashukuru sana wakulima Watanzania kwani wametuwezesha kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120 , 100 tunakula ndani 20 tunauza nje,”alisema

“Mwaka huu Tanzania tumeuza tani milioni moja laki moja Zambia na Congo DRC, nguvu na ruzuku tunazozitoa zinaturudishia fedha za kigeni nchini,” alisema.

Kuhusu Daraja alililozindua la Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 133 katika barabara ya Mikumi- Kidatu – Ifakara sehemu ya Kidatu – Ifakara kilometa 66.9 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Morogoro, Rais Samia alisema litawezesha kusaidia ufanyaji biashara kutoka sehemu moja kwenda sehemu ingine kwa urahisi na hivyo kuchochea uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema ndani ya mwaka huu wataendelea na uzalishaji sukari. Naye Waziri wa Viwanda, Sulleiman Jafo alisema mwaka 2021 nchi ilikuwa na viwanda 62, 385 lakini kwa kupitia sera nzuri za Rais Samia viwanda vimeongezeka hadi kufikia 80, 969 sawa na ongezeko la viwanda 18, 576 sawa na asilimia 22.9

Alisema katika sekta ya sukari waajiriwa wa moja kwa moja ni zaidi ya 26,000 ni zaidi ya 144,000 Pia aliwapongeza wakulima wa sukari Kirombero zaidi ya bilioni 67 zinaenda kwa wakulima kilombero.

Alimhakikishia Rais Samia kuwa uwekezaji wa sukari wanaupanua kwa lengo kubwa nchi ipate manufaa makubwa.