Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Serengeti
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii (Uhifadhi) Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu kupandishwa vyeo maofisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi.
Kamishna Wakulyamba alitoa pongezi hizo juzi wakati akifunga mafunzo ya uongozi kwa maofisa na askari wahitimu wapatao 236 katika hafla fupi iliyofanyika Fort Ikoma kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti ambapo maofisa walikuwa ni 159 na askari 77.
Akifunga mafunzo hayo, Kamishna Wakulyamba alisema; “Namshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuruhusu kupandishwa vyeo maofisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi. Pia namshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kunituma kumwakilisha katika hafla hii.” .
Aliwapongeza wahitimu na kuwataka maofisa na askari hao kuwa viongozi wa mfano na kuyaishi yale yote waliyojifunza wakati wakiwa mafunzoni.
“Elimu ni ujuzi unaokusaidia kutatua changamoto unazokutana nazo hivyo elimu mliyopata tuione ikiwasaidia kutatua changamoto mnazokutana nazo huku mkisimamia nidhamu na uadilifu ili jeshi letu la Uhifadhi liwe la mfano,” alisema na kuongeza;
“Mkafanye kazi kwa weledi na bidii mkifuata taratibu, kanuni, sheria na miongozo ya jeshi letu huku mkijiepusha na matendo yanayofedhehesha jeshi. Mkazingatie sheria na haki za binadamu.”
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa aliwapongeza wahitimu na wakufunzi wa mafunzo hayo na kusisitiza nidhamu na uwajibikaji kwa wahitimu hususani wanaporudi katika maeneo yao ya kazi.
“Mafunzo mliyoyapata yamewapa ujuzi wa kujieleza, kutafsiri sera na sheria za uhifadhi wa Wanyamapori na misitu, kuandaa mijadala na kusimamia mikakati mbalimbali ya kazi za uhifadhi na utalii.
Ni imani yangu kuwa mnaondoka hapa mkiwa tofauti na mlivyokuja,” alisema. Mwishawa aliongeza kuwa, Shirika linatambua kuwa mafunzo waliyopata yataongeza tija katika usimamizi wa rasilimali za nchi walizopewa dhamana ya kuzitunza na kuzilinda ili ziendelee kuchangia pato la Taifa.
Mafunzo hayo ya uongozi kwa maofisa na askari yamefanyika kwa awamu mbili yakilenga kuwajengea viongozi uwezo wa kusimamia nidhamu na kuimarisha mila na desturi za kijeshi ikiwa ni kwa nadharia na vitendo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best