Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Buhigwe
WAKAZI wa Kijiji cha Kilelema na Migongo katika Kata ya Kilelema Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wameridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ameleta neema kubwa ya maji katika kata yao.
Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari waliotembelea Kata hiyo juzi kujionea mafanikio waliyopata katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, wameeleza kufurahishwa na dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo.
Kevina Hamis (62) mkulima, mkazi wa Kilelema alisema tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 wakazi wa Kijiji hicho walikuwa hawajawahi kunywa ya maji ya bomba, lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani neema imewashukia.
“Tangu nchi ipate uhuru tulikuwa tunakunywa na kuoga maji ya mto ambayo siyo salama hali iliyopelekea watoto wetu na watu wazima magonjwa ya ngozi, kuhara mara kwa mara, lakini sasa hatuugui tena,” alisema.
Schola Chishako (45) mjasiriamali, mkazi wa Migongo ameeleza kuwa uongozi wa Mama Samia ni tofauti na marais wengine waliomtangulia, anajali sana maisha ya wakazi wa vijijini, hataki akinamama wateseke ndiyo maana amewapelekea maji.
“Miaka ya nyuma maji ya bomba yalikuwa yanapatikana Mijini tu, lakini tangu aingie madarakani Rais Samia ameleta neema kubwa, maisha ya wakazi wa vijijini hayana utofauti na wakazi wa Mijini, ameleta mageuzi makubwa,” alisema.
Akielezea hali ya huduma ya maji katika Wilaya hiyo Mtaalamu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo, Mhandisi Francis John Molel amemshukuru sana Rais kwa kuwapelekea fedha nyingi sana.
Alisema katika kipindi cha miaka 3 ya Rais Samia huduma ya maji safi ya bomba imefikishwa katika jumla ya vijiji 41 kati ya vijiji vyote 44 vilivyoko katika wilaya hiyo na hata vijiji 3 vilivyobakia mchakato wa kuleta maji umeshaanza.
“Rais Rais ameleta sh. mil 800 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji hapa Kilelema, mradi huu umefika asilimia 45, lakini pia ameshaleta zaidi sh bil 1 kwa ajili ya kutekelezwa mradi mkubwa wa maji katika Kijiji cha Migongo’, alisema.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitati ya Rais Samia hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama ya bomba katika Wilaya hiyo imeongezeka hadi kufikia asilimia 71 na kabla ya 2025 inatarajiwa kufikia asimia 85,”alisema.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM