November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia amaliza kero ya maji, wanawake wamshukuru

Na Allan Kitwe, Tabora,Timesmajiraonline

AKINAMAMA wanaoishi katika Kata ya Ntalikwa Wilaya ya Tabora wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na RAIS Samia Suluhu Hassan,  kwa kuwapelekea mradi wa  maji safi na salama ya bomba uliogharimu zaidi ya sh. mil 601.

Wakizungumza na gazeti hili kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi huo uliofanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava, wameeleza kufurahishwa na mradi huo kwa kuwa kata yao ilikuwa na shida kubwa ya maji.

Jesca Bhigendeka (40) mkazi wa Kijiji cha Ntalikwa alisema kuwa ujio wa mradi huo katika Kata yao umemaliza kero yao ya miaka mingi ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji ya kunywa na kupikia kwenye mabonde.

Alibainisha kuwa mradi huo ni mkombozi kwa familia zao kwa kuwa wanandoa wengi walikuwa hawana mahusiano mazuri kutokana na wake zao kuchelewa kurudi nyumbani mara kwa mara ikiwemo watoto wa kike kujiingiza katika mapenzi katika umri mdogo.

Sabrina Mohamed (42) maarufu kwa jina la mama wawili, mkazi wa Kijiji cha Magoweko alimshukuru Rais Samia kwa kuwaonea huruma akinamama na kutoa fedha za kutosha ili kuhakikisha mradi huo unakamilika haraka na kwa wakati.

‘Tunamshukuru sana Rais Samia, kwa kutujali akinamama na kutuletea miradi ya maji karibu na nyumbani ili tusihangaike kwenda kutafuta huduma hiyo umbali mrefu, hakika mama ametutua ndoo kichwani’, alieleza.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) Mhandisi Mayunga Kashilimu alisema kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya sh mil 601 utanufaisha jumla ya wakazi 4,264.

Alibainisha kuwa ujenzi wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya 6 kupitia Wizara ya Maji kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi waishio Mjini na Vijijini.

Mayunga alisema kuwa mradi huo ulioanza kutekelezwa Novemba 16, 2022 na kumalizika Novemba 11, 2024 unahudumia wakazi wa Vijiji 4 ambavyo ni Ntalikwa, Tumbi, Kakola na Magoweko.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na TUWASA, akaelekeza mradi huo kutunzwa vizuri ikiwemo kufanyiwa kazi maelekezo aliyotoa ili jamii inufike zaidi.