Penina Malundo, TimesMajira Online
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema ziara ya Rais wa Shirikisho la Watu wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, hapa nchini ni ishara njema kuhusu umuhimu wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili na inathibitisha dhamira yake ya kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria.
Rais Samia ametoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati yeye na mgeni wake wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya viongozi hao kumaliza mazungumzo ya faragha.
Rais Samia amesema jana asubuhi yeye na Rais Steinmeier, walipata fursa ya kuzungumza kuhusu masuala muhimu yanayohusu uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Ujeruman.
Kwanza, Rais Samia amesema wamezungumzia kuhusu ushirikiano wa kijamii na kiuchumi, ambapo uhusiano baina ya nchi hizo mbili umefikisha miaka 60.
Kwa mujibu wa Rais Samia katika kipindi chote hicho, nchi hizo zimekuwa zikishirikiana vyema.
“Serikali ya Ujerumani imekuwa ni rafiki, mbia mzuri ambaye tulishikana vizuri mkono katika mambo mengi, “amesema Rais Samia.
Ametaja sekta ambazo Tanzania ilifanyakazi na Serikali ya Ujerumani kuwa ni pamoja na masuala ya afya.
“Kama mnavyojua suala la Bima ya Afya tulitaka usaidizi kutoka kwao, lakini pia Serikali ya Ujerumani inajenga hospitali nzuri na kubwa sana ya Jeshi, pale Dodoma, lakini pia imetusaidia kujenga hospitali kubwa na ya kisasa ya maradhi ya kuambukiza Lugalo,” amesema Rais Samia.
Aidha, amesema Ujerumani imekuwa ikiisadia Tanzania katika masuala ya usambazaji maji safi na salama, masuala ya kilimo, elimu, elimu ufundi, utalii na utamaduni na michezo.
“Ulinzi tunashirikiana vizuri, maliasili na udhibiti wa fedha.” Amesema katika mazungumzo yao wamesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa nchi hizo na watu wake.
“Na katika hili, tumezielekeza timu za watalaam wa Tanzania na Ujerumani kuendelea na mazungumzo pamoja na mashauriano ya mara kwa mara yanayolenga kuboresha maeneo yaliyopo ya ushirikiano na kuibua maeneo mengine mapya yenye umuhimu wa kuinua uchumi wa nchi hizo mbili,”amesema Rais Samia.
Amesema katika hilo, amemhakikishia Rais Steinmeier kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya yajayo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwakani 2024.
Kwa upande wa biashara na mahusiano ya uwekezaji, Rais Samia alisema walizungumza na kusisitiza mchango wa biashara na uwekezaji katika kuchochea mchango mzima wa kijamii na kiuchumi, ambapo Ujerumani ina miradi 180 katika ngazi mbalimbali ambayo imewekezwa hapa nchini.
“Lakini pia tumekuwa tukifanya biashara na Ujerumani, ingawa bado kuna uwezekano mkubwa wa kukuza biashara na hilo watalielekeza kwenye mazungumzo yajayo,” amesema Rais Samia.
Amesema kwenye kongamano la wafanyabiashara baina ya Tanzania na Ujerumani, huko, ndiko fursa zote za uwekezaji na biashara zitaelezwa na pengine watakaokubaliana wataingia mikataba.
Rais Samia amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar, Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kijerumani katika kuandaa kongamano hilo ili kuwezesha biashara na kukuza uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wa utalii, Rais Samia amesema wamekuwa wakifanyakazi vizuri, wamekuwa wakipata watalii kutoka Ujerumani, lakini bado kuna uwezekano wa kupata idadi kubwa zaidi ya watalii kutoka Ujerumani pale watakapojitangaza vizuri kwao.
“Lakini tumekuwa tukishirikiana katika uhifadhi na mashirika mengine ya Ujerumani yamekuwa yakitusaidia katika uhifadhi wa mbuga zetu hasa Selou na Serengeti,”amesema Rais Samia.
Ametaja mambo mengi waliozungumza kuwa ni ya kihistoria, ambapo Tanganyika na Zanzibar kwa kipindi kidogo zilikuwa chini ya utawala wa Mjerumanina.
Amesema katika utawala huo, mambo mengi yamepita na walizungumza kwa urefu wakati wa mazungumzo yao.
Amesema wapo tayari kufungua majadiliano ya kuona jinsi ya kukubaliana wa yale yaliyopita nini wafanye. “Na nina jua kuna familia ambazo bado zinasubiri mabaki ya wapendwa wao, ambao wako Ujerumani katika makumbusho mbalimbali za Ujerumani, yote hayo tunaenda kuyazungumza na kuona vipi tuende nayo vizuri,” amesema.
Ameongeza kuwa Tanzania wanaangalia usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.
Rais Samia ameongeza kwamba; “Kwenye masuala ya demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora wamezungumza na Rais wa Ujerumani, Steinmeier amepongeza Tanzania kwamba Tanzania tunaonekana tumetulia kwenye utawala wa sheria, utawala bora, ndiyo maana wamevutika,”amesema.
Amesema ziara hiyo inathibitisha dhamira ya Serikali zote mbili za kuimarisha na kukuza ushirikiano wa urafiki wa nchi hizo kwa lengo la kunufaisha watu wetu.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza