Asema wananchi wanapata manufaa katika uzalishaji na huduma za kijamii
Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vya mkoa wa Shinyanga unaendelea vizuri na tayari umeanza kuleta manufaa kwa wananchi katika shughuli za uzalishaji na huduma za kijamii.
Amesema hali hiyo imeanza kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ambao sasa wanapata fursa ya kuboresha shughuli za kiuchumi pamoja na huduma muhimu za kijamii.

Naibu Waziri Salome ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kukagua utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vya Wilaya ya Kahama leo Machi 14,2026.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya umeme ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha, Salome amesema ataendelea kushirikiana na Waziri wa Nishati Mhe. Deograius Ndejembi katika kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha umeme unawashwa katika vitongoji vyote nchini.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata nishati ya uhakika ambayo itasaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuongeza uzalishaji pamoja na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta mbalimbali.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Bunge pamoja na Naibu Waziri walikagua na kuwasha umeme katika Zahanati ya Mine iliyopo Jimbo la Msalala pamoja na kuwasha huduma ya umeme katika mashine ya kusaga na kukoboa katika Jimbo la Kahama; Huduma ya umeme katika majimbo hayo imepatikana kupitia mradi wa kusambaza umeme vitongoji 15 kwa kila jimbo.

More Stories
CHAKUHAWATA yaiomba serikali kutoa maelekezo kwa waajiri
EWURA yatoa elimu uvunaji maji ya mvua kwa walemavu
Kamati ya Bunge yaridhishwa ujenzi kampasi ya Mzumbe