Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
KATIKA kukabiliana na makundi ya wanawake wanaofanya shughuli za kuuza miili yao maarufu kwa jina la “Nzige” kipindi cha msimu wa mavuno ya mazao vijijini, uongozi wa Serikali ya Kata ya Salawe katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga umetunga sheria ndogo itakayowadhibiti wanawake hao.
Hali hiyo imebainishwa na Ofisa mtendaji wa Kata ya Salawe, wilayani Shinyanga, Emmanuel Maduhu katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari wakati wa utekelezaji wa mradi wa Sauti za Kaya na vyombo vya habari unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (W.F.T).
Maduhu amesema wamefikia maamuzi ya kutunga sheria hiyo ndogo ili kuweza kuwabana wanawake wenye tabia ya kwenda vijijini kipindi cha mavuno kufanya biashara ya kuuza miili yao kwa malipo ya mazao ya magunia ya mpunga na wakati mwingine mahindi.
“Tabia ya wanawake hawa maarufu kwa jina la “Nzige” tumebaini ni chanzo kimojawapo cha wanawake wengi huku maeneo ya vijijini kufanyiwa vitendo vya ukatili, hii ni baada ya wanaume kuuza mazao waliyolima pamoja na baada ya kupata fedha wao hutokomea mijini na kutelekeza familia,”
“Ni jambo ambalo linaonekana kutaka kushamiri, mtu anatoka mjini na begi lake tu, anapanga chumba gesti, anaanza kujiuza kwa malipo ya mazao, mwisho wa msimu anatoka huku amejaza magunia ya mpunga kwenye Fuso, hii hapana tumeanza kuchukua hatua kupiga vita vitendo hivi,” anaeleza Maduhu.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kijiji cha Songambele kata ya Salawe walisema tabia ya wanawake kujiuza miili yao kwa malipo ya mazao imezoeleka katika maeneo mengi ya vijiji vya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambapo hata baadhi ya vijana ambao hawajaoa hulima mpunga kwa ajili ya kuja kuwapata wanawake hao.
Monica Mabilika na Mariamu Marco wamesema baadhi ya ndoa huvunjika inapofika kipindi cha msimu na chanzo huwa ni wanaume wanaouza mazao yote ya ndani bila kuwashirikisha wake au wenza wao hali inayozua mtafaruku mkubwa ndani ya familia na mara nyingine wanaume huhamia kwa “nzige” hao.
“Tunasikia kuna sheria ndogo inataka kutungwa kuwadhibiti hawa “Nzige” binadamu, kwa kweli itakomboa akina mama wengi maana hawa wanawake wenzetu hawatutendei haki hata kidogo, mtu unahangaika na mumeo kulima, halafu mkivuna mazao mwanaume anabeba na kwenda kuwaonga, laa inauma sana,” anaeleza Coretha Boniphace.
Akifafanua Coretha anasema iwapo kweli sheria hiyo ndogo itapitishwa itakuwa ni msaada mkubwa kwa wanawake wengi na watoto ambao mara nyingi wakuu wao wa kaya “wanaume” huwa na tabia ya kuuza mazao ya ndani bila kuwashirikisha na kisha fedha zote kuzimalizia kwenye starehe na machangudoa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato