November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sahara Sparks 2024 kufanyika Dar

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Sahara Ventures imetangaza rasmi tukio la Sahara Sparks 2024 ambalo lengo lake kuu ni kuwaleta pamoja wabunifu wa teknolojia, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo na teknolojia na kuwapa fursa ya kushiriki maonesho ya kibiashara pamoja na kujadili maswala mbalimbali ya teknolojia, maendeleo na uchumi. 

Kwa kutambua changamoto na pengo lililopo baina ya ujuzi unaohitajika na ule unaopatikana katika soko la ajira, Sahara Sparks inalenga kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuandaa mijadala mbalimbali itakayo ongeza ufahamu kuhusu changamoto hiyo na kuleta suluhu za kimkakati ikiwemo kuunda sera zitakazo saidia kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari mwishoni mwa wiki Mhandisi Samson Mwela, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) alitoa rai kwa  kampuni changa za ubunifu wa teknolojia (startups), sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo kushiriki kwenye maonesho na mijadala mbalimbali itakayo andaliwa katika wiki ya Sahara Sparks ambayo kilele chake kitakua tarehe 27-28 Septemba, 2024 kwenye ukumbi wa Mlimani city.

“Wiki ya Sahara Sparks imeandaliwa kwaa ajili yetu kwahiyo wote tushiriki hususani kampuni changa za ubunifu wa teknolojia zinazo fahamika kama Startups, sekta binafsi na wadau mbalimbali tutumie fursa hii kama njia ya kutangaza biashara zetu kwa kupitia maonesho yatakayo fanyika mlimani city mwezi Septemba mwaka huu, pia tushiriki mijadala ili kwa pamoja tutatue changamoto za ujuzi na ajira” alisema Mhandisi Mwela 

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike sambamba nakuhamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali alielezea umuhimu wa mijadala itakayo fanyika katika wiki ya Sahara Sparks 2024.

“Mwaka huu tutaandaa mijadala mbalimbali itakayo anagazia namna gani teknolojia, ubunifu na ujasiliamali unavyosaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa. Majadiliano haya yatatilia mkazo zaidi kuhusu rasilimali watu hususani vijana na jinsi ya kuwaandaa kwaajili ya ulimwengu mpya wa ajira.” alisisitiza Bw. Mtambalike.

Pia alizikaribisha sekta binafsi, startups, washirika wa maendeleo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watunga sera, wataalamu wa uvumbuzi na teknolojia, wajasiriamali na wadau wengine kushiriki tukio hili la kihistoria.

Kwa takribani miaka 9 sasa Sahara Sparks imekua ikifanyika kila mwaka na kwa mwaka huu inakuja na kaulimbiu ya “Watu, Ujuzi na Ulimwengu mpya wa ajira”.