Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Tanga
WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamechukua hatua za haraka kuona wananchi wa Kijiji cha Msomera kilichopo, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wanapata maji.
Kijiji cha Msomera kilikuwa kinakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 6,036 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Kufuatia ujio wa wananchi waliokubali kuhamia katika kijiji hicho kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, idadi yao imepanda hadi kufikia 17,000.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Juni 21, 2022 ofisini kwake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo alisema kwa ujio huo wa wananchi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, mahitaji ya maji yatakuwa makubwa, hivyo wameshachukua hatua za muda mfupi na mrefu.
“Kutokana na ujio wa wananchi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, kutafanya mahitaji ya maji katika Kijiji cha Msomera kufikia mita
za ujazo 450 kwa siku kwa kuzingatia matumizi ya wastani wa lita 25 kwa mtu mmoja kwa siku pamoja
na mahitaji ya maji katika taasisi.
“Kwa lengo la kuhakikisha wakazi waishio katika Kijiji cha Msomera wanapata huduma ya maji safi na salama ambayo ni toshelevu, Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imefanya utafiti wa vyanzo vya maji vya uhakika
ambavyo vitawezesha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kiasi kisichopungua mita za ujazo
450 kwa siku” alisema Mhandisi Lugongo.
Lugongo alisema vyanzo ambavyo vilionekana vitaleta matokeo mazuri ni vyanzo vya maji juu ya ardhi
kupitia ujenzi wa bwawa na vyanzo vya maji chini ya ardhi kupitia uchimbaji wa visima virefu. Kazi ya uchimbaji wa visima virefu ilianza kwa kufanya tafiti ambapo Bodi ya Bonde la Pangani na
Kampuni ya Wema Consult Limited zilifanya tafiti ya maji chini ya ardhi na kisha kazi ya uchimbaji
kuanza.
Alisema hadi sasa jumla ya visima 18 vimechimbwa, ambapo kati ya hivyo visima vitano vilipata
maji. Baada ya kufanya vipimo vya ubora wa maji katika visima hivyo vitano, visima vinne (4) vilipata
maji yanayofaa kwa matumizi, ambapo visima vilivyochimbwa vina uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo
2.5, tatu, 7.8 na 19.8, na hivyo kuwezesha upatikanaji wa maji jumla ya mita za ujazo 775.2 kwa siku.
Mhandisi Lugongo alisema Serikali kupitia RUWASA imeingia Mkataba na Kampuni ya CHELESI GENERAL ENTERPRISES LTD ya Mafinga mkoani Iringa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la maji kwa thamani ya sh. bilioni 1.99. Utekelezaji wa mkataba
huo ni wa miezi 12.
“Hata hivyo matarajio ni kazi hii itakamilika kabla ya muda uliopangwa. Utekelezaji wa mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 9.8. Kazi zinazotegemewa kufanyika katika mkataba huu ni kusafisha eneo la mradi,
kuondoa tuta lililokuwa limebomoka,
kuchimba msingi wa tuta (Core trench) wenye urefu wa mita 357, ujenzi wa tuta lenye urefu wa mita 357, ulazaji wa bomba la kupitisha maji lenye kipenyo cha milimita 350, kupanga mawe kwenye uso wa tuta upande wa juu, kupanda nyasi kwenye uso wa tuta upande wa chini.
“Ujenzi wa vituo viwili vya kuchotea maji, ujenzi wa mbauti mbili kwa ajili ya kunyweshea mifugo, ambapo kazi ambazo zimefanyika hadi sasa
ni kusafisha eneo la ujenzi wa bwawa, na imekamilika kwa asilimia 100, kuondoa tuta lililokuwa limebomoka imekamilika kwa asilimia 100, uchimbaji wa msingi wa tuta (Core trench) pamoja na kuchonga mianguko (Side slopes)
umekamilika kwa asilimia 49″ alisema Mhandisi Lugongo.
Lugongo alisema mpango wa muda mfupi wa kuwawezesha wananchi wa Kijiji cha Msomera kupata maji umefanyika, wakati utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa bwawa na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji
katika kijiji hicho ukiendelea, ambapo RUWASA tayari imekwisha jenga miundombinu ya maji ambayo inawezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Kijiji cha Msomera kwa baadhi ya maeneo.
“Kazi ambazo zilipangwa kufanyika ni uwekaji wa mfumo wa umeme unaotumia nishati ya jua, ufungaji wa pampu moja katika kisima, ujenzi wa mnara wa tanki wenye kimo cha mita sita, uwekaji wa tanki la plastiki juu ya mnara lenye ujazo wa lita 10,000, ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kisimani hadi kwenye tanki, uunganishaji wa maji katika vituo vinane (8) vya kuchotea maji (vilula). Kazi ambazo zimekwisha fanyika ni uwekaji wa mfumo wa umeme unaotumia nishati ya jua umekamilika kwa asilimia 100, ufungaji wa pampu moja katika kisima umekamilika kwa asilimia 100.
“Ujenzi wa mnara wa tanki wenye kimo cha mita sita umekamilika kwa asilimia 100, uwekaji wa tanki la plastiki juu ya mnara lenye ujazo wa lita 10,000 umekamilika kwa asilimia 100, ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kisimani hadi kwenye tanki umekamilika kwa asilimia 100, na uunganishaji wa maji katika vituo 8 vya kuchotea maji umekamilika kwa asilimia 100, ambapo kupitia ujenzi wa miundombinu hii ya muda, kumewezesha upatikanaji wa maji katika vituo vinane (8) ambavyo
vimekwisha unganishwa” alisema Lugongo.
Alisema kwa sasa ujenzi wa mnara wenye kimo cha mita tisa unaendelea kujengwa , ambapo matanki mawili yenye ujazo wa lita 10,000 kila moja yatawekwa katika mnara huo ili kuwezesha,upatikanaji wa maji katika eneo kubwa.
Aidha kwa kuwa baadhi ya makazi yapo mbali na vituo hivyo vinane (8) ambavyo vinatoa huduma. Na kwa kuwa
katika nyumba zilizojengwa kumewekwa matanki yenye ujazo wa lita 1000, wakazi wanaoishi katika makazi hayo wanawekewa maji katika matanki hayo kwakutumia gari (Water bowser) na wakazi hao wataendelea kupata huduma ya maji kupitia utaratibu huo hadi miundombinu inayoendelea kujengwa
itakapokuwa imekamilika na kuwezesha wakazi hao kupata maji kupitia vituo vilivyojengwa.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini