January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA Tabora wawezeshwa vitendea kazi vya Mil 934

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

SERIKALI imetoa magari 5 na pikipiki 48 vikiwa na thamani ya zaidi ya sh mil 934 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani Tabora ili kuboresha utendaji kazi wa Wakala huo na Vyombo vya Watoa Huduma kwa Jamii (CBWSOs) katika wilaya zote.

Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imefanyika juzi katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na kuhudhuria na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Meneja wa RUWASA Mkoa, Mameneja wa Wilaya, Watumishi na Wasimamizi wa Vyombo vya Watoa Huduma kwa Jamii (CBWSOs).

Akikabidhi vifaa hivyo Mkuu wa Mkoa Balozi Dkt Batilda Salha Burian amewataka Watumishi wa Wakala huo na Wasimamizi wa CBWSOs ngazi ya jamii kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za maji kwa wananchi.

Amebainisha kuwa magari hayo 5 ambayo yamegharimu zaidi ya sh mil 800 na pikipiki 48 zaidi ya sh mil 130 ni vitendea kazi muhimu sana kwa Wakala huo kwa kuwa vitachochea weledi wa sekta ya maji katika Mkoa huo.

‘Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya 6 chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kununua magari na pikipiki hizi kwa lengo la kuboresha utoaji huduma ya maji katika vijiji vyote vya Mkoa wetu’, amesema.

Dkt Batilda ameongeza kuwa serikali imetoa fedha nyingi sana katika sekta hiyo ili kuhakikisha kero ya maji katika Mkoa huo na Mikoa mingine nchini inabakia historia, hivyo akawataka watumishi kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza lengo la Mheshimiwa Rais la kumtua mama ndoo kichwa.

Amesisisitiza kuwa vitenda kazi hivyo vinaenda kuongeza nguvu katika usimamizi, uendeshaji na usambazaji miradi ya maji katika kata na vijiji vyote vilivyoko katika mkoa huo.

Naye Meneja wa RUWASA Mkoani hapa Mhandisi Hatari Kapufi ameeleza kuwa vitendea kazi hivyo vitasaidia sana kupunguza changamoto ya vyombo vya usafiri kwa watumishi na Viongozi wa Vyombo vya Watoa huduma katika ngazi ya jamii.

Amebainisha kuwa magari hayo aina ya Landcruiser hard top na pikipiki aina ya Hero hunter CC 125 vilivyonunuliwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 vitagawiwa katika wilaya zote za Mkoa huo.

Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wametenga bajeti ya ununuzi wa magari mengine 5 na pikipiki 18 ambavyo vitaenda kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto iliyopo sasa ya vyombo vya usafiri kwa Wakala huo.

Mhandisi Kapufi ameeleza kuwa katika kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na RUWASA Mkoani hapa inakuwa endelevu wamesajili jumla ya vyombo 62 vya watoa huduma ya maji katika ngazi ya jamii (CBWSOs).

Amesema katika jitihada hizo za kuboresha utendaji kazi jumla ya vyombo 27 vya watoa huduma vimepatiwa vyombo vya usafiri (pikipiki), vyombo ambavyo havijapata ni 35 navyo vitapatiwa usafiri huo kwa mwaka huu wa fedha.

Amemshukuru Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Naibu wake Mary Prisca Mahundi na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo na timu yake kwa kazi nzuri wanayofanya ili kuhakikisha sekta ya maji inaboresha huduma zake kwa asilimia 100 katika Mkoa huo.