January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ruvuma yakamilisha ujenzi wa jengo la huduma za dharura (EMD)

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya maboresho katika sekta ya afya na kuhakikisha wananchi huduma katika vituo vya afya zinatolewa kwa wakati na zenye ubora nchini.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino Serikalini Wizara ya Afya Bi. Catherine Sungura wakati wa ziara yake na waandishi wa habari wa Mkoa wa Ruvuma walipotembelea utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya huduma za dharura (EMD) na wagonjwa mahututi (ICU).

Bi. Sungura amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya afya ikiwemo ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya huduma za dharura pamoja na wagonjwa mahututi katika hospitali za rufaa za mikoa nchini.

Amesema kuwa kwa Mkoa wa Ruvuma shilingi Millioni 630 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa la wagonjwa wa dharura pamoja na shilingi Millioni 152 ya ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi.

Amesema majengo yote ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 na yataanza kutumika hivi karibuni.

Ameongeza kusema kuwa kukamilika kwa majengo hayo kutasaidia wananchi wa mkoa huo pamoja na nchi jirani kupata huduma ambapo awali hawakuwa na jengo hilo.

“Vilevile jengo hilo la wagonjwa mahututi litakua na huduma za hewa tiba pamoja na mashine za kisasa za kusaidia upumuaji na kuimarisha ufuatiliaji wa tiba ya mgonjwa mahututi,” amesema.