Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma
ALIYEWAHI kuwa mtumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Abdulhakim Kabuga amehukumiwa kulipa faini ya shilingi 500,000 au kwenda jela miaka mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma Sostenes Kibwengo amesema mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani na TAKUKURU kwa kosa la kupokea hongo ya sh.30,000 ili amsaidie mtoa taarifa kupata kitambulisho cha Taifa mapema.
Aidha Mahakama ya Wilaya ya Kondoa imemuhukumu mtendaji wa Kata ya Thawi Hashim Ally Mohamed kulipa faini ya sh. 300,000 au kifungo cha miaka miwili .
Mahakama hiyo imetoa hukumu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi kwamba mtuhumiwa huyo alishawishi rushwa ya shilingi 175,000 na kupokea shilingi 80,000 ili asimchukulie hatua mzazi ambaye hakumpeleka binti yake sekondari baada ya kufaulu.
Katika hatua nyingine Kibwengo amesema,TAKUKURU imeokoa shilingi 45.760 milioni alizolipwa Mkandarasi wa kampuni ya Leostart Engineering ya jijini Dar es Salaam alizolipwa mkandarasi kinyume na utaratibu wa utekelezaji wa mradi wa maji wa kijiji cha Mlongila wilayani Chemba fedha hizo ni sehemu tu ya fedha alizolipwa mkandarasi huyo.
“Mtakumbuka siku za nyuma tuliwahi kuwataarifu kuhusu ufuatiliaji wetu wa mradi huo na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ulionyesha kuwa Mkandarasi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 579.323 ulioanza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2014 alilipwa fedha zaidi ya kazi zilizofanyika na hivyo kutakiwa kuzorejesha.” amesema Kibwengo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua