Na Penina Malundo, timesmajira
IMEELEZWA kuwa kutokuwepo kwa uwazi na kuona aibu kwa waathirika wa rushwa ya ngono wengi imetajwa kuwa ni moja ya sababu inayochangia vitendo vya rushwa ya ngono kuongezeka nchini hususan maeneo ya maofisini,vyuoni na kwenye vyama vya siasa.
Pia matukio hayo yanaonekana kukua na kuongeza kasi kwa sasa hususan kwa wasichana wengi ,licha ya uripotiwaji wake kutoendana na kasi ya matukio hayo.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative,Rebecca Gyumi wakati wa majadiliano ya kuhusu rushwa ya ngono kwa wasichana yaliyohusisha wadau kutoka taasisi na mashirika mbalimbali,ikiwa ni muendelezo wa kusherekea siku ya wanawake duniani.
Gyumi amesema kinachowafanya wasichana wengi kutoripoti visa wanavyokutana navyo pindi wanapooneshwa viashiria vya kuombwa rushwa ya ngono ni pamoja na usiri wanaokuwa nao kwa kuhofia haki yao kutopata au kutojua mahali wanapoweza kwenda kushtaki.
Amesema ripoti  kuhusu suala la rushwa ya ngono hazipo kwa kiasi kikubwa na hata zinapotoka inaonekana hakuna upatikanaji wa haki ambayo itafanya matukio hayo kuweza kupungua.
”Suala la rushwa ya ngono ni suala lililojikita katika mifumo ya mahusiano ya kinguvu kwa mtu wenye mamlaka kutumia mamlaka yake kwa mtu asiyekuwa na mamlaka ambapo tukiangalia katika tamaduni za jamii zetu nyingi, katika kujua maamuzi ya msichana kuwa yeye ni nani na anataka nini utakuta kuna watu wanakuwa sehemu ya kumfanyia maamuzi hali inayofanya yeye kushindwa kupaza sauti,’amesema na kuongeza
”Na hata wanapopaza sauti utakuta hawa watu wenye nguvu au mamlaka tayari wameshikilia hatima yao ikiwemo elimu na fursa ya ajira hivyo inakuwa ni ngumu kushindana na mfumo huo,”amesema.
Aidha amesema katika taasisi ambazo zinamamlaka ya kuhakikisha suala hili la rushwa ya ngono linapotokea na wao wanalifanyia kazi ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ( PCCB),bado wananchi wengi wamekuwa nyuma kufahamu kama kuna sheria au vifungu ambavyo vinakatazwa rushwa ya ngono kama moja ya rushwa.
”Bado wananchi hawafahamu pindi wanapokutana na viashiria au tayari ameombwa rushwa ya ngono kutokujua wapi wanaripoti,kwa nani na namna gani watapata msaada,bado taasisi hizi zinakazi ya kufanya katika hili”amesema.
Gyumi amesema ikija suala la taasisi zinazotoa haki bado maamuzi nayo uchelewa na kutotoka kwa wakati hali inayofanya mtoa taarifa kushindwa kujiamini licha ya kujua eneo alilopo ndio sehemu ambayo wangeweza kukimbilia.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Center for Strategic Litigation,Deus Rweyemamu amesema katika tafiti walizofanya sio tu kwa Tanzania bali kwa afrika zimeonyesh wapo wasichana wengi wangependa kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi lakini wamekuwa wakikumbwa na vikwazo vya rushwa ya ngono.
Amesema wanawake wamekuwa wanakutana na vikwazo vingi iwe maofisini ,vyuoni,sehemu za biashara,pamoja na kwenye siasa.
”Tunachukua jitihada nyingi lakini bado ndoto hazifikiwi kwa wasichana na wanawake wengi kutokana na vikwazo kwa baadhi ya watu wenye mamlaka,”amesema na kuongeza.
”Kitendo cha binti au mwanamke kushindwa kufikia ndoto yake kwa sababu tu kuna mbaba au mkaka anamtaka ni kosa kubwa,”amesema.
Naye Mmoja wa waathirika wa rushwa ya ngono kutoka moja ya Chuo Kikuu nchini,Mariam Yusuph(sio jinalake halisi)amesema mwaka 2019 alipokuwa mwaka wa pili chuoni mwalimu wake alianza kumfatilia na kumpigia simu hata muda wa chuo kuisha.
Amesema mwalimu huyo aliweza kuwa na ushawishi kwake hali ambayo hata kipindi cha mitihani yake kilikuwa kigumu kutokana na kutomkubali kuwa naye kimahusiano.
”Licha ya kukumbana na vikwazo hivyo kwa walimu wawili tofauti lakini nilibaki na msimamo wangu na kuhakikisha najituma kusoma na kujithamini hadi nilifanikiwa kumaliza chuo na kufaulu vizuri bila kuishi nao walimu wote wawili,”amesema
More Stories
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa