October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rukwa yafanya uhakiki maeneo ya wazi, umma

Na Abdulrahman Salim,TimesMajira Online. Rukwa

OFISI ya Ardhi Mkoa wa Rukwa, inaendelea na zoezi la kufanya uhakiki wa maeneo ya wazi na ya umma yaliyoorodheshwa kwa mujibu wa ramani za mipango miji za halmashauri za mkoa huo, ili kubaini endapo kuna uvamizi umefanyika katika maeneo hayo.

Akizungumza kuhusiana na zoezi hilo Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Rukwa, Swagile Msananga amesema lengo la kufanya zoezi hilo ni kupata orodha kamili ya meneo ya wazi, ili yaweze kutambulika rasmi huku akiwaonya wananchi waliovamia katika maeneo hayo.

“Kwa maeneo ambayo yatakuwa yamevamiwa, kutakuwa hakuna namna ya kufanya isipokuwa wavamizi wataondolewa, ili kupisha maeneo ya wazi kwa sababu yanatakiwa yalindwe kwa nguvu zote na maeneo ambayo yapo salama mpaka sasa hivi, tutahakikisha mipaka yake inawekwa bayana na wananchi watatakiwa waiheshimu,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya kupata orodha kamili ya maeneo hayo atakabidhiwa Mkurugenzi, ili aweze kuyaandalia hati kwa ajili ya ulinzi wa maeneo hayo kwa siku za usoni.