May 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC Kuzaga awataka askari kudumisha nidhamu

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewataka askari 208, waliyovishwa  Vyeo kudumisha nidhamu
katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku na kuleta mabadiliko chanya ndani ya Jeshi la Polisi.

Kamanda Kuzaga amesema hayo Mei, 23,2025 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura wakati wa kuwavisha vyeo Askari Polisi 208 ngazi ya Koplo, Sajenti na Sajini Meja wa Polisi.

Aidha, Kamanda Kuzaga amesema kuwa, Jeshi hilo linatambua mchango wa kila Askari na litaendelea na utaratibu wake wa kupandisha vyeo na kutoa zawadi mbalimbali kwa Askari kutoka na utendaji unaozingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu.

Mmoja wa Askari aliyevishwa cheo Sajini Meja wa Polisi Benson Lucka wa Polisi Wilaya ya Mbeya amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura kwa kuwapendekeza na kuwapandisha vyeo kutokana na utendaji kazi wao.

Askari hao wamevishwa vyeo baada ya kupendekezwa na kisha kuhudhuria na kuhitimu mafunzo ya uongozi mdogo katika vyuo na Shule ya Polisi Tanzania (TPS) zamani ikijulikana CCP iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro.