December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Royal Tour yajaza nyumba za wageni mikoani

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Waziri wa uwekezaji viwanda na biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema mahoteli katika Mikoa ya Daresalaam, Arusha na Kilimanjaro yamejaa kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo kutokana na filamu ya Royal tour aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hasan ya kuhamasisha utalii nchini.

Pia amewataka wafanyabiashara Mkoani Tanga kuchangamkia fursa za watalii wanaoingia nchini kwa kutoa huduma zenye viwango vinavyohitajika.

Wageni wengi wanakuja nchini baada ya kuvutiwa na filamu aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na waziri wa uwekezaji, viwanda na biashara Dkt. Ashatu kijaji wakati wa maonyesho ya 9 ya biashara na utalii yanayofanyika jijini Tanga na kusema kuwa filamu ya the royal tour imeleta ushawishi kwa wawekezaji na watalii kuja nchini ambapo amewataka wafanyabiashara kujenga hoteli za kisasa na kutoa huduma zinazohitajika.

Ametoa rai kwa watanzania kujipanga kikamilifu katika kuchangamkia fursa, mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga hoteli nzuri zenye viwango kwajili ya malazi ya watalii, wawekezaji na wafanyabiashara ndani ya Taifa huku akiitaka jamii kujiandaa kwa pamoja kwajili ya kupokea watalii nchini.

“Hoteli zote zimejaa kwa miezi mitatu ijayo hivyo nimewaambia umoja wa mahoteli hapa Tanga mnaposikia majirani zenu wote hawana nafasi ya kuhudumia kilichobaki mbele yako ni wewe kujipanga vizuri na sasa ni jiji la Tanga na mahoteli yake kupokea eatalii na wawekezaji, “amesisitiza waziri Kijaji.

Aidha waziri huyo amewataka wafanyabiashara kujipanga kikamilifu kuhakikisha huduma wanazotoa zinatoka kwa kiwango kinachokubalika na kujua bidhaa wanazouza ni za kiwango gani.

Amesema wizara yake kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii wamejiandaa vizuri kuona wanashirikishana kwenye fursa hizo ili watanzania ambao ni wafanyabiashara ili waandae mazingira ambayo ni wezeshi kwa kuelezana yale yote yanayohitajika ili hatimaye waweze kunufaika na fursa hizo zilizoletwa na Rais kupitia filamu ya the Royal tour.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuona uchumi w kupitia bishara, utalii unakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa.

Waziri Kijaji amesema takwimu zinaonyesha uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa pato la taifa kwa Tanzania umeongezeka na kufikia asilimia 35 jambo ambalo limeonyesha mwamko mkubwa.

Hivyo kupitia maonyesho hayo ya 9 ya biashara na utalii waziri huyo amemuahidi Rais kuwa ndani ya miaka yake mitatu kwenye uongozi wake wa awamu ya kwanza kuwa wanataka wafikie China ikiwezekana wawapite kwakuwa taifa letu lina vivutio vingi na fursa nyingi za uwekezaji.

“Katika kufikia hayo nini serikali yetu ya awamu ya sita imefanya tumeweza kuridhia mkataba wa eneo huru la biashara la Afrika ndani ya soko huru hili la Afrika timeingia mkataba wa kwenda kuuza bidhaa zetu kwenye nchi 54 na sisi tukiwa wa 55,”alibainisha waziri huyo

Waziri Kijaji amewasisitiza watanzania kuzalisha bidhaa za kiwango cha kimataifa ili kuweza kupambana kwenye soko la ushindani.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amesema kuwa lengo la maonyesho hayo ya tisa ni kutoa elimu ya biashara na ujasiriamali kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga.

“Nikuambie tu wazi mheshimiwa waziri Tanga tuna tabia ya kutojithamini sisi wenyewe mwaka jana yale makampuni makubwa ambayo hayakushiriki tumeburuzana kwa nguvu na yameweza kushiriki kikamilifu mwaka huu nimesema wazi kavisa haya, makampuni makubwa ambayo hayatki kukaa na kushiriki katika maonyesho haya lakini biashara zao na pesa zao wanapata kupitia Tanga basi wasiwe sehemu ya ofisi yangu, “alisistiza Malima.