Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
MFANYABIASHARA maarufu na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini, Rostam Azizi, ameungana na Watanzania wengine kulaani vikali mauaji ya kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mohamed Kibao, yaliyotokea hivi karibuni.
Katika tamko lake,Rostam ameelezea masikitiko yake makubwa kufuatia tukio hilo la kikatili, akisema ni hatua ya kurudi nyuma kwa Taifa.
“Nchi yetu imejengwa kwenye misingi ya utu, uhuru na haki. Matukio ya kikatili kama haya hayapaswi kupewa nafasi katika jamii yetu,”amesema Rostam katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Rostam ametoa pole kwa familia ya marehemu pamoja na wanachama wa CHADEMA akisisitiza kuwa ametiwa moyo na hatua za haraka zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye ameagiza uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu tukio hilo na matukio mengine kama hayo.
“Namuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa ujumbe wake mzito alioutoa kwamba nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Ni muhimu kama taifa tusimame imara kuhakikisha kuwa vitendo vya kikatili vya aina hii vinakomeshwa kabisa,”amesema Rostam.
Rostam, ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini, ametoa wito kwa Watanzania wote kushikamana na kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa kwa kila mtu.
“Tusiruhusu kurudi nyuma kwenye giza la ukosefu wa utu na thamani ya maisha ya binadamu,”amesema.
Ameeleza kuwa tukio hilo la mauaji limeleta mshtuko mkubwa nchini, huku wananchi wengi wakitaka haki itendeke haraka iwezekanavyo.
“Hii ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya utekaji na utesaji ambayo yamekuwa yakiripotiwa nchini katika siku za hivi karibuni,”amesema.
Katika kumalizia tamko lake, Rostam amesisitiza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kushiriki katika kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kutawala nchini.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari