Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online
WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kushirikiana na Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) katika mapambano ya dawa hizo, kwani vita hiyo ni ngumu hivyo DCEA haitakiwi kuachwa peke yake.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba, wakati akitoa mada kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kupambana na dawa za kulevya kwenye semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na DCEA.
Semina hiyo ya siku mbili imemalizika jana jijini Dar es Salaam.
Amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kushirikiana na DCEA katika mapambano ya dawa za kulevya ikiwemo vile vya maudhui (mitandaoni) kwani mchango mkubwa kwenye vita hiyo.
Dkt. Rioba, amesema tafiti zinaonesha biashara na matumizi ya dawa za kulevya inaongezeka Afrika, huku Tanzania ikiongoza kwa Afrika Mashariki kwenye mapambano ya dawa hizo kutokana na hatua mbalimbali inazochukua ikiwemo kuteketeza.
Ameongeza kuwa, vyombo vya habari vikiamua vinaweza, ingawa vinakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo uelewa mdogo wa dawa za kulevya na changamoto zake.
Ametaja nyingine ni ujuzi mdogo wa kufuatilia habari za kiuchunguzi, gharama kubwa za kufanya habari za uchunguzi na ufuatiliaji, uhalifu wa kupangwa na gharama za maisha ya mwandishi, kutokana na uwezo walionao wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Changamoto nyingine kwa mujibu wa Dkt. Rioba ni mbinu za biashara kubadilika kuendana na teknolojia.
Ameshauri wanahabari wapewe elimu kuhusu dawa za kulevya na namna ya kuripoti habari za uchunguzi kuhusu dawa hizo, vyombo vya habari vifuatilie watumiaji na vifanye uchunguzi ili kujua wafanyabiashara wa dawa hizo.
Aidha, alishauri vifanyike vipindi vya watu kuonesha watu walioacha dawa za kulevya, ili kutumia elimu hiyo kusaidia elimu badala ya kuonesha wale wanaojidunga.
Dkt. Rioba alitoa ushauri mwingine kwa vyombo vya habari akivitaka vishirikiane na vyombo vingine kama DCEA, kwani wao wana mengi wanayojua, hasa kwa kutambua kwamba vyombo vya habari vimeyumba kwa kupungukiwa na kipato.
Amesema, vyombo vya habari vinaweza kushirikiana kuchunguza na kufuatilia wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza