January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RIKOLTO yawajengea uwezo wasambazaji wa pembejeo vijijini na waganikazi mkoa wa Songwe

Na Moses Ng’wat, Songwe.

WAMILIKI wa maduka madogo ya pembejeo za kilimo na Waganikazi 35 wa Mkoa wa Songwe wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya viuatilifu na mbolea, lengo likiwa ni kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya wakulima, pamoja na uhakika wa chakula.

Mafunzo hayo ambayo yamewakutanisha wadau hao wa kilimo kutoka wilaya zote za Mkoa wa Songwe, yametolewa na shirika lisilo la kiserikali la Rikolto kwa kushirikiana na Agra na kufanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Julai 24, 2024, mtaalamu wa kilimo biashara kutoka shirika hilo la Rikolto, Praygod Malisa, amesema Rikolto inatekeleza Mradi wa mwaka mmoja kwa kuwajengea uwezo wamiliki wa maduka madogo ya pembejeo yalioyopo maeneo ya vijijini pamoja na waganikazi.

Malissa amesema sababu kubwa ya utekelezaji wa mradi huo ni kujaribu kuwapunguzia wakulima gharama za uzalishaji na kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao matano ya kimkakati ambayo ni Maharage, Soya, Mahindi, Mpunga, pamoja na mazao ya mboga mboga.

“Pamoja na kuwajengea uwezo wamiliki wa maduka ya pembejeo na Waganikazi, lakini pia tunaenda ‘kusapoti’ wachakataji na waongeza thamani ili kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija , pia kuongeza uzalishaji na kuwa na uhakika wa chakula” amesema Malissa.

Katibu Tawala msaidizi Mkoa wa Songwe upande wa uchumi na uzalishaji, Vansica Kulanga, amesema mafunzo hayo kwa waganikazi yana manufaa makubwa kwa mkoa wa Songwe ambao ni mwa mikoa mikubwa ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwani watasaidia kuwafikia wakulima waliopo pembezoni hasa katika matumizi ya mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Wilayani Songwe , Yahana Simkanga, amesema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa kuwa wakulima wengi hawana uweleza wa kutosha katika matumizi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo hali ambayo hufanya uzalishaji kutokuwa na tija.

Rikolto kwa sasa inatejeleza mradi huo katika mikoa mitatu ya Nyanda za juu kusini ambayo ni Ruvuma, Mbeya na Songwe.