November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rekodi ya kihistoria miaka mitatu ya Rais Samia

*TIC yasajili miradi ya trilioni 38.3/-, aifanya Tanzania kuongoza kwa mazingira bora ya uwekezaji Afrika, vivutio vya kikodi usipime

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo yamekiwezesha kusajili miradi 1,188 yenye thamani ya sh.trilioni 38.3 katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake na kuifanya Tanzania kuongoza kwa mazingira bora ya uwekezaji Afrika.

Kati ya miradi hiyo iliyosajiliwa, asilimia 35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ni ya wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Gilead Teri, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kituo hicho kwenye kipindi hicho.

Amesema kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2024, TIC imesajili jumla ya miradi 1,188 sawa na ongezeko la asilimia 63.19 ikilinganishwa miradi 728 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho, Machi 2018 hadi Machi 10 2021.

Amesema kwenye ajira zilizozalishwa kutokana na usajili wa miradi kumekuwa na ongezeko la asilimia 231.63 kutoka ajira 104,172 zilizozalishwa kipindi cha miaka mitatu ya kuanzia mwaka 2018 mpaka 2021 mpaka ajira 345,464 zinazotarajiwa kuzalishwa katika kipindi cha miaka mitatu ya awamu ya sita kuanzia Machi 2021 mpaka Machi 2024.

Amesema kumekuwa na ongezeko la usajili wa miradi kutoka nje linatokana na juhudi zinazofanywa na Rais Samia katika kuitangaza nchi na kuhamasisha uwekezaji kupitia Sera maalum ya ushirikano kupitia Diplomasia ya kiuchumi.

Amesema ongezeko la miradi linatokana na ushiriki wa Tanzania katika makongamano mbalimbali nje ya nchi na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini

Teri amesema tathmini inaonesha kuwa idadi kubwa ya miradi iliyosajiliwa ipo katika sekta za kipaumbele ambazo ni uzalishaji viwandani miradi 538, usafirishaji miradi 225, utalii miradi 110, sekta ya ujenzi wa majengo ya biashara miradi 106 na Kilimo miradi 106.

Teri amesema Tanzania inaendelea kuwa kinara Afrika Mashariki katika kupokea wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini na kwamba hiyo imetokana na mabadiliko yaliyofanywa kwa kuleta sheria mpya na bora ya uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2022.

Mkurugenzi amesema Sheria za uwekezaji zina nafasi muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kuchagiza wawekezaji kwani imeweza kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja FDI zaidi nchini Tanzania.

Amesema vivutio vya kikodi na Sheria mpya za uwekezaji zinatoa vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyokuwa vya kodi ili kuhamasisha uwekezaji wa ndani na wa kigeni na kwamba vivutio hivyo vinajumuisha vivutio vya kodi kwa wawekezaji wa kawaida na wa kimkakati.

Teri amesema matarajio ya TIC kwa mwaka wa 2024, ni kusajili miradi 1,000 ya uwekezaji, katika kipindi cha msimu wa 2024 na kuweka malengo ya kuvutia mitaji ya kigeni yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tano na kuvutia mitaji ya ndani ya Dola za Marekani bilion 3.5.

Amesema pia TIC imejipanga kuhakikisha kwamba, angalau asilimia kumi ya miradi iliyosajiliwa inalenga katika kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuonyesha jitihada za kituo hicho za kusukuma mbele uwekezaji wenye manufaa na endelevu.