December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA yasaini mikataba na wakandarasi kupeleka umeme vituo vya afya na vituo vya maji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) leo, Novemba 21, 2022 umesaini mikataba na wakandarasi watatu watakaotekeleza Mradi wa kupeleka umeme vijijini katika vituo vya afya na visima vya maji.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ndiye aliyesaini mikataba hiyo akiiwakilisha Serikali, akishuhudiwa na Mwakilishi kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Styden Rwebangila pamoja na Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Mhandisi Francis Songela ambao wameufadhili Mradi.

Tukio hilo limefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam na kuzihusisha kampuni za wakandarasi za OK Electrical and Electronics Services Limited itakayotekeleza Mradi huo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Katavi, Kigoma, Shinyanga na Tabora.

Kampuni nyingine ni Stategrid Electrical and Technical Works Ltd itakayojikita katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Rukwa, Songwe, Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma.

Vilevile, Kampuni ya Dieynem Co. Limited itatekeleza Mradi huo katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida, Geita, Kagera, Mara, Mwanza na Simiyu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Saidy ameeleza kuwa Mradi utahusisha kupeleka umeme katika hospitali 6, vituo vya afya 57 na visima vya maji 363 katika maeneo mbalimbali vijijini.

Amefafanua kuwa Mradi unafadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama zinazokadiriwa kuwa shilingi bilioni 24.6 na utatekelezwa kwa miezi tisa katika mikoa 25 ya Tanzania Bara ukiondoa Dar es Salaam.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu amewasisitiza wakandarasi waliosaini mikataba hiyo kuzingatia utendaji kazi wenye viwango, kasi na tija ili kuleta matokeo chanya kama walivyojipambanua katika Maandiko yao ya kuomba kazi hiyo.

“Tumieni vifaa vyenye ubora katika kutekeleza Mradi. Hatutarajii kukutana na nguzo zilizopasuka. Mnalazimika kukidhi vigezo vya TANESCO katika suala la ubora wa kazi na sisi tutawafuatilia kwa asilimia 100. Kwa upande wetu, tutatimiza wajibu wetu ipasavyo,” amesema.

Amemalizia kwa kuwasisitiza wakandarasi, ambao wote ni wa ndani, kutoiangusha Serikali ambayo imeendelea kuwaamini kwa kuwapatia kazi mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Rwebangila amesema utekelezaji wa Mradi huo ni sehemu ya mikakati ya Serikali katika kuhakikisha huduma muhimu za umma zinapewa kipaumbele katika kufikishiwa nishati ya umeme.

“Miradi hii ya vituo vya afya na visima vya maji ni sehemu ya huduma muhimu kwa wananchi. Ili huduma hizo zitolewe kwa ufanisi kwa wananchi ni lazima kuwe na umeme. Ndiyo maana miradi hii inaenda kutekelezwa ili kuvifikia vituo husika ambavyo bado havina umeme,” amefafanua.

Naye Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Mhandisi Songela amesema Ofisi hiyo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA kwa malengo ya kuwafikishia huduma adhimu wananchi waishio vijijini. Amesema, huduma za afya pamoja na maji ni miongoni mwa huduma muhimu kwa binadamu ndiyo maana wakaona ni vema watoe ufadhili katika kutekeleza mradi husika.

Akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi waliotia saini mikataba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya O.K. Electrical & Electronics Services Ltd, Mrisho Masoud, aliahidi kutekeleza kwa viwango kazi hiyo walioaminiwa na Serikali kuwa wanaweza kuifanya.

Mkurugenzi Mkuu ametoa shukrani kwa Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya nishati vijijini ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wananchi.

Mradi wa kupeleka umeme vijijini katika vituo vya afya na visima vya maji utatekelezwa kwa miezi 9 katika mikoa yote ya Tanzania Bara ukiondoa Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kushoto), akibadilishana kabrasha za mikataba na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya O.K. Electrical & Electronics Services Ltd, Mrisho Masoud, baada ya kutia saini mikataba ya kupeleka umeme vijijini katika vituo vya afya na visima vya maji, Novemba 21, 2022 Dar es Salaam. Wanaoshuhudia na Mwakilishi wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila (wa pili-kushoto) na Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya ambao wamefadhili mradi huo, Mhandisi Francis Songela.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (wa pili-kushoto), akisaini mkataba na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya O.K. Electrical & Electronics Services Ltd, Mrisho Masoud (wa pili-kulia) unaohusu kupeleka umeme vijijini katika vituo vya afya na visima vya maji, Novemba 21, 2022 Dar es Salaam. Wanaoshuhudia na Mwakilishi wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila (wa tatu-kushoto) na Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya ambao wamefadhili mradi huo, Mhandisi Francis Songela. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa REA, Mussa Muze.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akizunguza katika hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa Mradi wa kupeleka umeme vijijini katika vituo vya afya na visima vya maji. Mikataba hiyo ilisainiwa baina ya REA na Wakandarasi, Novemba 21, 2022 jijini Dar es Salaam.