Na Mwandishi wetu,Tanga,timesmajira
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zinazolenga kuboresha eneo la kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, wilayani Handeni, ambalo ni makazi mapya ya wananchi wanaohamia kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Hayo yamebainishwa jana wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo aliyefuatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy wilayani Handeni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Viongozi hao wamesema REA imeunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kuhakikisha wananchi wanaohamia eneo hilo wanapata nishati ya umeme ambayo ni muhimu kwa kila mtu.
“Mpango wa Serikali kuwaomba baadhi ya wakazi wa Ngorongoro kuhamia katika eneo hili umefanya mahitaji ya nishati kuwa makubwa kuliko bajeti tuliyoipanga awali; hivyo tumetembelea tujionee mahitaji halisi ili tukapitishe nyongeza ya bajeti itakayokidhi mahitaji ya wananchi wote wa eneo hili,” amesema Wakili Kalolo
Amesema , upelekaji umeme umehusisha pia kuongeza wigo kwa wakazi wa vijiji jirani ambao walikuwa hawajafikiwa na nishati hiyo ili nao wafaidi huduma hiyo na kuboresha hali ya maisha.
Amefafanua zaidi, Mkurugenzi Mkuu wa REA, amesema tayari ujenzi wa kilomita 23 kati ya 30 za njia ya kupeleka umeme katika eneo husika zimekwishakamilika na transfoma iko tayari kuwashwa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Saidy ameeleza kuwa Serikali imeahidi kutoa pesa kwa ajili ya kuongeza wigo wa upelekaji umeme kwa kilomita mbili zaidi kwa kila kijiji ili kuongezea kilomita moja ya awali ambayo kimsingi ilikuwa na lengo kuu la kufikisha umeme mkubwa katika kila kijiji.
“Kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo yote ya Tanzania, wasiwe na hofu kwani ile kilomita moja ni ya awali, lakini kila kijiji kitapata kilomita mbili za ule umeme mdogo na hivyo tunatarajia tutafikia wateja wengi zaidi,” amesisitiza.
Mhandisi Saidy ameongeza kuwa,, REA inatekeleza pia Mradi wa Ujazilizi ambapo jumla ya vitongoji 85 vimekwishafikiwa na huduma na kuna ongezeko la vijiji 51 zaidi ambavyo pia vitapatiwa umeme kupitia Mradi husika mkoani humo.
Amesema, kuna jumla ya Kandarasi Sita zinazotekelezwa mkoani Tanga, ambazo alizitaja kuwa mbili kati yake ni za Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Kandarasi Tatu ni za Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na Kandarasi Moja ni ya Mradi wa ujazilizi.
Naye Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhandisi John Sallu, ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa imekuwa mstari wa mbele katika kuwapambania wananchi katika kuhakikisha mazingira wanayoishi yanakuwa bora zaidi ikiwemo kuwapelekea nishati ya umeme.
Akieleza zaidi, Sallu amebainisha kuwa, katika Jimbo lake kasi ya utekelezaji wa miradi ya REA inakwenda vizuri na kwamba kupitia ziara ya viongozi wa REA, baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na upungufu yametolewa ahadi ya kufikishiwa nishati ya umeme.
Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera, Martin Oleikayo Parakett amemshukuru Mungu, Rais Samia pamoja na viongozi walio chini yake hususan wa Wizara ya Nishati, REA na TANESCO kwa kuona umuhimu wa kukipelekea kijiji hicho umeme.
Ametoa rai kuwa nishati hiyo itolewe kwa usawa kwa wakazi wote ambao wanajumuisha wenyeji pamoja na wageni wanaohamia.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini