December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA kuipatia umeme shule ya Chifu Hangaya, Magu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeahidi kugharamia gharama zote za kuunganisha umeme katika Shule ya Msingi ya Chifu Hangaya wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, inayojengwa kwa ufadhili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ikumbukwe Rais Samia alisimikwa kuwa Chifu Mkuu wa Machifu Tanzania wakati wa Hafla iliyofanyika Agosti 8, 2021, katika Viwanja vya Red Cross eneo la Kisesa, wilayani Magu na kupewa jina la Chifu Hangaya, hivyo shule hiyo imepewa jina lake.

Ahadi hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Rachel Kassanda, akiwa ameongoza Ujumbe wa Bodi katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini wilayani humo.

Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi aliofuatana nao, ambao ni Mhandisi Styden Rwebangila na Florian Haule, Mwenyekiti huyo amesema REA inaunga mkono jitihada za Rais Samia za kuwaletea wananchi maendeleo hivyo itafadhili uunganishaji umeme ili ndoto yake njema kuona watoto wote wanapata elimu bora itimie.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Janet Mbene akizungumza wakati wa kikao kifupi baina ya Bodi na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Rachel Kasanda (hawapo pichani) kujadili utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya aliishukuru REA kwa ahadi hiyo akisema kuwa nishati ya umeme itawezesha shule hiyo iliyo katika hatua za mwisho kukamilika kutoa elimu bora kwa watoto.

Katika hatua nyingine, Bodi imeahidi kuzisaidia kaya maskini zaidi, hususan zile zilizoko katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ambazo zimefikiwa na miradi ya umeme vijijini, kwa kuzipatia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) bure ili kuwawezesha wakazi wake kuepuka gharama za kutandaza nyaya katika nyumba zao.

Aidha, Bodi imetoa hamasa kwa Maafisa Uchumi na Mipango wa Wilaya kote nchini, kuainisha fursa zilizoko katika maeneo yao kwa wananchi ambao wamefikiwa na miradi ya umeme vijijini ili waitumie nishati hiyo kuchangamkia fursa hizo kwa ajili ya kuinua hali yao kiuchumi.

Msimamizi wa Miradi ya Nishati Vijijini Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ernest Makale (aliyesimama kushoto), akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo wilayani Magu wakati wa kikao kifupi baina ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Rachel Kasanda.

Awali, Ujumbe wa Bodi ulifanya ziara katika Wilaya ya Ilemela ambapo ulikutana na Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Masala pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali.

Bodi imeahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazohusu umeme vijijini zilizowasilishwa na viongozi hao wa Wilaya za Ilemela na Magu ili kuhakikisha azma ya Serikali kuwapatia wananchi maendeleo kupitia nishati hiyo inafikiwa kikamilifu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoani Mwanza, Mhandisi Ernest Makale, jumla ya miradi sita ya umeme vijijini inatekelezwa katika Mkoa huo ambapo ikikamilika itakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi.

Bodi ya Nishati Vijijini inaendelea na ziara katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini ambapo katika hatua za awali, imeeleza kuridhishwa na kasi ya Wakandarasi inayoleta matumaini kuwa itakamilika kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Rachel Kasanda (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Mhe, Janet Mbene (wa tatu-kulia), baada ya kikao kifupi kujadili utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini Septemba 6, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Makale, Wajumbe wa Bodi Florian Haule na Mhandisi Styden Rwebangila pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Romanus Lwena.