Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amepongeza Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga kwa kupata shilingi bilioni 38 ikiwa ni fedha za ziada kutoka Benki ya Dunia (WB) baada ya kufanya vizuri kwenye miradi ya Lipa kwa Matokeo (PforR).
Mkoa wa Tanga umeishinda mikoa mingine 24 ambayo ilikuwemo kwenye kinyang’anyiro cha kufanyiwa tathmini na Benki ya Dunia kwa fedha walizotoa awali kwa mikoa hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, ndipo Tanga walipofanya vizuri kwenye utekelezaji wa miradi hiyo,hivyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, RUWASA Tanga itaanza ‘kumwagiwa’ fedha hizo sh. bilioni 38.
Ameyasema hayo Juni 19, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuunganisha Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) kwenye Mfumo wa Kielektroniki (Maji IS Billing System) wa utoaji ankara za maji na ukusanyaji wa mapato (Maji IS na GePG), ambapo mafunzo hayo yanafanyika mjini Lushoto kwa siku 14 na baadhi ya viongozi wa CBWSO 50 za mkoa huo wanashiriki.
“Niwapongeze RUWASA Mkoa wa Tanga hasa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo (Lugongo) kwani umefanya kazi kubwa, na kuwezesha Mkoa wa Tanga kuongoza mikoa mingine kwa kupata fedha za ziada sh. bilioni 38 baada ya kufanya vizuri kwenye miradi ya maji ya Lipa kwa Matokeo (PforR).
“Kwa kupata fedha hizo, Mkoa wa Tanga utaweza kutekeleza miradi mingi ya maji, na kuweza kutoa huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi hasa waliopo vijijini, na kuweza kutimiza adhma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mwanamke ndoo kichwani,”amesema Dkt. Burian.
Dkt.Burian amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza makusanyo ya mapato serikalini, kwani hadi kufikia Machi, mwaka huu katika mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia CBWSO’s, wameweza kukusanya sh. milioni 290.9 hivyo ni matumaini yake kiasi hicho cha fedha kitaongezeka mara mbili.
“Nimeambiwa kuwa kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka Januari hadi Machi, 2024 mmekuwa na Vyombo vipatavyo 50 kwenye mkoa na mmeweza kukusanya sh. 290,948,440,hivyo ni matumaini yangu kuwa makusanyo haya yataongezeka mara dufu baada ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya huduma ya maji” amesema Dkt. Burian.
Dkt. Burian amesema takwimu zinaonesha kuwa huduma ya upatikanaji maji kimkoa imefikia asilimia 59 ambayo sawa na idadi ya watu wapatao 1,126,338 wanaopata huduma ya maji kwa umbali wa mita 400 katika Mkoa wa Tanga.
Ambapo vijiji vyenye huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 55 ya mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 77 ya sasa ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.
“Aidha, kazi ya kuhakikisha maeneo yote ya vijijini yanafikiwa na huduma ya maji safi na salama bado ni kubwa ikizingatiwa kuwa hadi kufikia Disemba 2025 tunatakiwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji uwe umefika asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na hii ni kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020/2025.
“Hivyo, mkisimamia skimu za maji vizuri kutakuwa na uhakika wa ongezeko la makusanyo ya fedha na hivyo kusaidia katika kuimarisha uendelevu wa huduma na kufikia malengo kwa kiasi kikubwa ya kumtua mama ndoo kichwani” amesema Dkt. Burian.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa kwa sasa wanakusanya sh. milioni 96 kwa mwezi kupitia CBWSO’s, lakini kupitia mfumo wa GePG wataweza kukusanya sh. milioni 150 kwa mwezi, hivyo kuweza kukusanya sh. bilioni 1.8 kwa mwaka.
Mhandisi Lugongo amesema pia wanakwenda kuhakiki watumiaji wa maji, kusimamia ukusanyaji wa mapato ili miradi ya maji iwe endelevu.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, alimuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa watafanya kazi kubwa iliyotukuka itakayoendana na thamani ya fedha ili kufikia malengo yaliyowekwa na Rais Dkt. Samia ya kumtua mwanamke ndoo kichwa.
Mkoa wa Tanga ndiyo mkubwa nchini kiutawala ukiwa na wilaya nane (8), halmashauri 11, majimbo ya ubunge 12, na kata 245.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato