Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online Tanga,
BARAZA la madiwani wa Halmashauri ya jiji la Tanga limemuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba kuingilia kati suala la viongozi wa chama na madiwani kuswekwa rumande wakihusishwa na tuhuma mbalimbali ambapo wamedai jambo hilo linakivua nguo chama cha mapinduzi ccm.
Ombi hilo limetolewa na Mstahiki Meya wa jiji hilo Abdulrahman Shiloo wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Tanga wa kupitia na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Meya Shiloo amesema kuwa ndani ya miaka miwili hii wamepata kadhia ya viongozi wao wanne kuswekwa rumande ikiwemo madiwani watatu na Mwenyekiti wa wazazi ambaye hivi sasa ni mjumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa lakini pia ni mjumbe wa kamati ya maadili ya Mkoa.
“Ndugu zetu mnapotufanyia hivi mnaweza mkaona upande wa kwanza mnafanya kazi zenu lakini mnakivua nguo chama, mnatuvua nguo sisi na kesho mnatufanya tunakuwa hatuna nguvu ya kwenda kuitetea hii serikali kwasababu mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mwenyekiti wa wazazi wilaya anawekwa ndani eti kwasababu tu kakutwa na gari inashutumiwa imeibiwa kumbe wala gari haijaibiwa ilikuwa imewekwa bondi na aliyekuwa nayo bondi ni mtu anayeaminika na gari ilishapelekwa kituoni kibaya zaidi Mwenyekiti wetu akakosa dhamana licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kujidhamini, “amesisitiza Meya Shiloo
Ameongeza kuwa Mkuu wa Mkoa kinavhosikitisha zaidi diwani ametoka kumzika mama yake jana siku ya pili anakamatwa anawekwa ndani yaani inasikitisha inatukatisha sana tamaa hatukatazi mamlaka zifanye kazi yake tunataka zifanye kazi yao vizuri kwasababu CCM inataka viongozi wasafi lakini mnapokwenda kumkamata mtu ambaye ni diwani na kusema kwamba sio raia habari hizi zinatapakaa kwamaana ya kwamba kumbe chama cha mapinduzi hakiko makini katika kuteua viongozi wake, “amesema Meya
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kufanikiwa kupunguza idadi ya hoja za ukaguzi zinazojadiliwa kwa mwaka huu, kulinganisha na zilizojadiliwa mwaka jana, ambapo kwa mwaka huu ni hoja 41, tofauti na mwaka jana zilikuwa hoja 44.
Amesema ni jambo la kujipongeza kwa kupunguza idadi ya hoja, kwani zipo Halmashauri zingine hoja zimeongezeka, na hivyo kuzitaka Halmashauri za Mkoa wa Tanga kuhakikisha zinapiga hatua kwa kupunguza hoja, na kuondoa hoja za kujitakia kwa kila mmoja kusimama katika nafasi yake.
“Tumepiga hatua kidogo kwa kupunguza wingi huu wa hoja kutoka 44 mwaka jana mpaka 41 mwaka huu nimesema maneno haya wakati nilipokuwa napita kwenye Halmashauri zingine wewe fanya chochote lakini upige hatua usiwe vile vile tuu kila wakati wengine hoja zimeongezeka lakini nyinyi mmeweza kupunguza hoja japo kwa uchache hivyo niwaombe mjipongeze natarajia mwakani zishuke zaidi ya hapa, “amesema Mkuu wa Mkoa.
Aliongeza kuwa hakuna sababu ya kurudi nyuma twende tukapange mikakati mbinu mbalimbali kwa vipawa ambavyo Mwenyezi Mungu ametujaalia tukiwa naimani ndani ya miaka mitatu tunaweza kusimama mahali tukasema tulikuwa hapa na sasa tuko hapa na mipango yote na mikakati inasukwa tukiwa hapa Tanga jiji tukiamini hili ndio jiji, “
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amewataka watendaji wa Halmashauri ya jiji hilo kutekeleza wajibu wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutenda haki kwa wananchi na badala yake wasiwe chanzo cha migogoro kwenye maeneo yao.
Katika makusanyo yake ya mapato ya ndani Halmashauri ya jiji la Tanga imefanikiwa kufikia asilimia 92 ya makisio yake ambapo Mkuu wa Mkoa Tanga amewataka watendaji kuongeza jitihada ili kufikisha asilimia mia moja au na zaidi katika wiki mbili zilizobaki kukamilika kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
More Stories
Nani kuwa mrithi wa Kinana CCM?
Watendaji Songwe wapatiwa mafunzo uboreshaji daftari la mpiga kura
Samia: Mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio