Na Allan Vicent, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati amewataka wazazi na walezi mkoani humo wanaoficha watoto wenye ulemavu kuacha mara moja tabia hiyo vinginevyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali.
Alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akihamasisha wananchi wa tarafa ya Simbo wilayani Igunga Mkoani Tabora kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli imetoa fursa kwa watoto wote kupata elimu bure pasipo kulipa gharama yoyote kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne, hivyo kila mtoto anapaswa kupelekwa shule.
Amesisitiza kuwa mzazi au mlezi yeyote atakayeficha mtoto wake mlemavu au kutompeleka shule atakumbana na dola na mkondo wa sheria utachukua nafasi yake ili kumlinda mtoto huyo na kumwezesha kupata elimu.
Amesema kuwa kila mtoto aliyetimiza miaka 6 au 7 anatakiwa kuanza shule bila kubanguliwa kutokana na hali yake ya kimwili na kuongeza kuwa kutompeleka shule mtoto mwenye ulemavu ni kosa kisheria.
RC Dkt.Sengati amepongeza juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na wadau wa elimu ikiwemo Shirika la World Vision katika mkoa huo kwani zimewezesha kuboreshwa kwa mazingira ya shule, upatikanaji elimu na ukuaji salama wa watoto.
Aidha amefafanua kuwa mabaraza ya watoto yaliyoundwa yamewawezesha kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao katika suala zima la ulinzi na usalama wa mtoto ikiwemo kutambua haki zao za msingi, na kueleza yanayowakabili kupitia maadhimisho mbalimbali ikiwemo siku ya mtoto wa Afrika .
Amebainisha kuwa hadi sasa watoto takribani 2,600 wameingizwa katika ufadhili wa mtoto na kuwajengea mtandao wa mawasiliano na wafadhili mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia kujiendeleza kielimu.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ