November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Tabora akamata vitabu vinavyohamasisha ushoga

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Paul Matiko Chacha amepiga marufuku Taasisi isiyo ya kiserikali ya Kapuya Foundation kwa kuleta vitabu na vifaa mbalimbali vya elimu ikiwemo komputa ambavyo vinahamasisha ushoga kwa watoto mashuleni.

RC Chacha ametoa maelekezo hayo juzi Wilayani Kaliua Mkoani hapa alipokuwa akiongea na wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo Viongozi wa chama na serikali, wataalamu na wakazi wa wilaya hiyo.

Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikijishughulisha na utoaji msaada wa vifaa vya elimu hususani vitabu, komputa na taulo za kike katika shule za msingi na sekondari katika Wilaya hiyo na maeneo mengine hapa nchini.

‘Miongoni mwa vifaa walivyokuwa wakigawia vijana wetu wa shule za msingi na sekondari tumebaini kuwa vinahamasisha vitendo vya ushoga na usagaji, jambo ambalo ni hatari sana, hivyo kuanzia leo hii Taasisi naifuta hapa Tabora’, amesema.

RC Chacha amesisitiza kuwa Taasisi hii haina nia njema kwa watoto wetu walioko mashuleni, kwani kuwagawia vitabu vinavyohamasisha ushoga na usagaji maana yake wanataka vijana wote walioko mashuleni wawe mashoga na wasagaji.

Amebainisha kuwa Mratibu wa Taasisi hiyo licha ya kutakiwa kuja kwenye mkutano huo alidai kuwa anaumwa, lakini RC akaagiza akamatwe mara moja kokote kule aliko hata kama amelazwa hospitalini apigwe pingu.

Aidha ameagiza Taasisi hiyo ifungashe vilago na isionekane tena katika wilaya hiyo na Mkoa mzima na vifaa vyote walivyokuwa wakigawa visipokelewe tena na vile vilivyokwisha kabidhiwa viteketezwe kwa kuwa hawana imani navyo.

Chacha amefafanua kuwa Taasisi hii ililetwa Kaliua kwa ajili ya kugawia vijana wa shule za msingi na sekondari zote zilizopo Mjini Kaliua vitabu na komputa, ila kwa uharibifu huu uliomo ndani ya vifaa vyao hatutaki kitu chao chochote kile.

Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Rashid Chuachua amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya Taasisi hiyo na kubainisha kuwa watateketeza kila kifaa walichokileta na watahakikisha haifanyi kazi yoyote katika Wilaya hiyo.