January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Songwe aagiza mkaguzi wa ndani, msaidizi wake kupewa ulinzi na Polisi

Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Tunduma.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dk.Francis Michael, ameliagiza jeshi la polisi Wilayani Momba kuwapa ulinzi Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Mji Tunduma na msaidizi wake kutokana na vitisho walivyoanza kuvipata baada ya kutoa ripoti ya ukaguzi ambayo imesababisha watumisi sita wa Halmashauri hiyo kuchukuliwa hatua za kufukuzwa kazi.

Alitoa agizo hilo juni 17,2023 kwenye kikao cha Baraza maalum la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Tunduma kwa ajili ya kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha wa 2021/22.

Alisema mkaguzi wa ndani wa Halmashauri hiyo, Engelbert Maro na msaidizi wake Thomas Mzee, waanze kupewa ulinzi kwa sababu ana taarifa kuwa watendaji hao wameanza kupewa vitisho na kumtaka Mkuu wa polisi wilaya (OCD), John Lwamlema, kuanza kutekeleza agizo hilo mara moja .

“Kamanda wa polisi mkoa leo (juzi) hatuko nae hapa, lakini wewe OCD uko hapa nataka huyu mkaguzi wa ndani na msaidizi wake uhakikishe wanalindwa…maana nina taarifa kuwa wanatishwatishwa” alisisitiza Mkuu wa Mkoa Dk. Michael

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza wewe mkuu wa idara ya ukaguzi na mwenzako… yule rafiki yangu (Thomas Mzee) mmefanya kazi nzuri sana kwenye ripoti yenu ya ukaguzi kwa sababu kuna watumishi wanafikiri fedha zinazoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni za kugawana”.

Wiki iliyopita, baraza la Madiwani katika Halmashauri hiyo ya Mji Tunduma iliwafukuza kazi watumishi sita, huku wengine wawili wakikumbwa na adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kupatikana na makosa mbalimbali yakiwemo ya ubadhirifu.

Baraza hilo la Madiwani pia lilimshusha wadhifa Mkuu wa idara ya Kilimo wa Halmashauri hiyo, Ronald Msangi, huku watumishi wengine wanne wakinusurika baada ya kushindwa kupatikana na hatia katika makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayoub Mlimba aliwambia wandishi wa habari kuwa, baraza hilo lilifikia uamuzi huo kufuatia hoja zilizoibuliwa na madiwani katika baraza lililopita la mwezi wa Disemba mwaka 2022.

Aliwataja watumishi wa ajira za kudumu waliofukuzwa kuwa ni Mkuu wa kitengo cha manunuzi wa Halmashauri hiyo, Obeid Mwakalinga, Ofisa manunuzi daraja la pili, Ibrahim Lulimo, Mhandisi daraja la pili, Aly Farayo, pamoja na Dickson Kisemine ambaye ni mhandisi daraja la pili.

Watumishi wengine wawili waliofukuzwa kazi ambao walikuwa kwenye ajira za mkataba katika Halmashauri hiyo kuwa ni Aly Hasan ambaye alikuwa Mhandisi wa majengo, pamoja na Japhet Chota ambaye alikuwa Mhadisi ukadiriaji majenzi katika Halmashauri hiyo.

Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mlimba alisema katika kikao hicho, watumishi wawili ambao ni Patricia Mbigili ambaye ni Ofisa elimu Sekondari katika Halmashauri hiyo na Raphael Simkonda (ofisa Mtendaji daraja la tatu) wao wamepewa adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao katika kipindi cha mwisho.