Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameipongeza Kampuni ya PASS Leasing kwa kuwawezesha wakulima kupata matrekta ambayo yanawasaidia kwa shughuli za kilimo.
Senyamule ametoa pongezi hizo jijini hapa leo, Agosti 7, 2024 wakati alipofika kukabidhi matrekta 10 kwa wakulima yaliyotolewa kama mkopo na kampuni hiyo ambayo inawakopesha wakulima hao, na wanapomaliza deni, trekta linakuwa ni mali ya mkulima.
“Niwapongeze PASS Leasing kwa kuweza kuwakopesha wakulima kwa kulipa kidogo kidogo na wanapomaliza deni inakuwa ni mali yao,jambo hilo nimelipenda sababu linamsaidia mkulima, kwani hata kama hana pesa, anachofanya ni kuweka kidogo kidogo na kuweza na yeye kumiliki trekta lake” almesema Senyamule.
Senyamule amesema azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepanga kuwaaminisha Watanzania kuwa kilimo hakina msimu, na hiyo ni kutokana na kujenga mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo kwa kampuni ya PASS Leasing kutoa matrekta kwa wakulima, ni kuunga mkono juhudi hizo za wakulima kulima wakati wote.
“Katika Maonesho haya ya Nanenane kitaifa, tunaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo kwa ajili ya wenzetu Pass Leasing ambao wamewawezesha wakulima kupata mikopo ya vifaa vya kilimo ili waweze kufanya shughuli zao kwa kutumia teknolojia na utaalamu zaidi badala ya kutumia nguvu na mikono,haya ni mapinduzi makubwa na yanaungana moja kwa moja na mipango ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka ile kilimo ni Uti wa Mgongo iwe kwa vitendo.
“Wao wakulima wenyewe wanaendelea kujua umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa katika Sekta ya Kilimo,tumeshuhudia wadau wakiamini na wakiungana na Serikali kuhakikisha wakulima wanapata teknolojia, na leo tunaziona jitihada za kumuunga mkono Rais zinazofanywa na PASS Leasing katika Sekta ya Kilimo” amesema Senyamule.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Leasing Company Ltd Kilo Lusewa alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa hiyo ni kampuni tanzu inayomilikiwa na PASS TRUST, iliyosajiliwa mwaka 2019 kwa sheria za makampuni ya Tanzania na inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania. Lengo kuu la kampuni hiyo ni kusaidia Sekta ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kwa kutoa mikopo ya zana za kilimo na viwanda bila dhamana yeyote na kwa masharti nafuu ili kuwawezesha wakulima kuongeza tija na thamani ya mazao wazalishayo ili waweze kufikia malengo yao.
“PASS Leasing ni kampuni pekee ya kitanzania ambayo imejikita kwenye shughuli za ukopeshaji/ ukodishaji wa zana na viwanda mbalimbali vya uchakataji katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Kutokana na unafuu wa masharti inayofanya tofauti na watoa huduma wengine, kwa kuwawezesha zana za kilimo na viwanda kwa hadi asilimia 80 ya gharama bila dhamana. Taasisi ya PASS Leasing kwa kipindi cha miaka mitatu ya utendaji imefanikiwa kuwafikia wakulima zaidi ya 1,000 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Na kuwawezesha zana zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 50 nchini kote. Kati ya hao vijana ni asilimia 20, wanawake ni takribani asilimia 10. Kampuni hii imefanikiwa kutoa vifaa mbalimbali ikiwemo trekta, powertiller (trekta za mikono), mashine za kuvunia, mashine za kuchakata mazao, magari ya usafirishaji wa mazao ya kilimo na vifaa mbalimbali vinavyotumika kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, uvuvi na ufugaji” amesema Lusewa
Lusewa amesema katika hafla hiyo
Kampuni ya PASS Leasing, imekabidhi vifaa vya kulimia, ambavyo ni trekta tisa aina ya New Holland TT75-4WD, machine ya kupura mahindi na gari moja aina FAW zenye themani ya sh. milioni 755.5 kwa wakulima wa mkoa wa Dodoma na Singida; waliowezeshwa kupitia huduma za PASS Leasing.
Uwezeshaji huo wanategemea utakwenda kuongeza uzalishaji kwa kulima mashamba zaidi ya ekari 4,000 na ujenzi na usambazaji wa kiwanda cha viwatilifu; kutengeneza ajira za moja kwa moja zisizopungua 65 na kuwafikia wanufaika takribani 700 kwa kipindi cha msimu mmoja . Aidha, katika kanda ya Kati, mkoa wa Dodoma na Singida wameshawezesha zana zenye jumla ya thamani ya takribani ya sh. bilioni 20 kwa wajasiliamali takribani 400 kati yao vijana ni asilimia 25.
“PASS Leasing imekuwa na makubaliano ya kibiashara na kampuni ya HUGHES AGRICULTURE TANZANIA, GF Trucks na Imara Tech ambao ni wauzaji na wasambazaji wa zana mbali mbali za kilimo ikiwemo trekta ,mashine za kuchakata mazao, vyombo vya usafirishaji na zana nyingine.Makubaliano haya yanalenga kuhakikisha wakulima wajasiriamali wanapata bidhaa bora, na huduma baada ya mauzo ikiwemo mafunzo na huduma za utengenezaji wa zana.
“Hadi kufikia sasa kwa kushirikiana na kampuni hii tumeweza kwa pamoja kutoa zana mbalimbali zaidi ya 600, ambazo zipo kwenye ubora wa juu na wakulima wanafurahia huduma zao na Kampuni hizi zinahudumia wateja nchi nzima kupitia matawi yaliyopo Dar es salaam, Arusha ,Morogoro, Dodoma,na Kahama” amesema Lusewa.
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano