Na Anthony Ishengoma,Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati ametembelea miradi mitatu yenye thamani ya shilingi milioni 528 inayoendelea katika Manispaa ya Shinyanga wakati wa kuadhimisha siku 100 za uongozi  wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
 Akiongea na vyombo vya habari wakati wa ukaguzi miradi hiyo, Dkt. Sengati amesema, kwa kipindi cha siku 100 Rais Samia Suluhu Hassan tayari ametoa kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Kitangiri, milioni 50 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Ngokoro na milioni 528 za ujenzi daraja linalounganisha Kata ya Kitangili na Kata ya Chamagua zilizoko Manispaa ya Shinyanga.
Dkt. Sengati ameongeza kuwa, Rais Samia alitoa fedha kwa miradi hiyo kama hatua muhimu ya kuunga juhudi za wananchi ambao tayari walishaanza juhudi za ujenzi wa miundombinu ya shule pamoja na Kituo cha Afya na kusema kuwa kama watu wanakuwa na uelewa kuanzisha miradi yao, Serikali lazima ichangie katika juhudi hizo.
‘’Kiashiria kikubwa cha maendeleo kwa namna yoyote ile ni kiwango kikubwa cha uelewa wa wananchi, ndio maana Rais ameendelea kuwekeza katika Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo vya kati na vya juu kwa kuweka fedha nyingi sana hivyo tuendelee kuunga mkono jitihada hizi,”ameongeza Dkt. Sengati.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ya Iwelyangula, Robert Munyereshi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuleta fedha haraka kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Iwelyangula linalounganisha Kata ya Kitangiri na Kata ya Chamagua na hivyo kuweka matumaini ya kuondokana na adha kubwa ya kukosa usafiri hasa baada ya daraja la awali kukatika na kuifanya mawasiliano yao kuwa magumu.
Mzee Munyereshi ameongeza kuwa, kama Serikali itaendelea na juhudi hizi basi maendeleo ya Taifa hili yatakwenda kwa kasi sana akiwapongeza pia uongozi wa Manispaa na wilaya kwa kuwa weledi na wenye haraka katika kushughulikia maendeleo ya wananchi.
Wakati huo huo, Damaris Nyantabano mkazi wa Kata ya Ngokoro alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuwa, baadhi ya wanawake jirani na sekondari hiyo wamejitolea nguvu zao na kushiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo ili kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan mkono katika kuleta maendeleo, lakini pia wanafanya hivyo kwa faida ya watoto hao ambao watatumia madarasa hayo hapo baadae.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Yasinta Mboneko alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuwa miradi hiyo inayoendelea ilianza na nguvu ya wananchi na kuweza kuinua jengo la Kituo cha Afya na baadae Serikali kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kuongezea nguvu za wananchi kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati ametembelea miradi hiyo kama hatua ya awali ya kuadhimisha siku 100 za utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na mchango wake kwa maendeleo ya Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi