Na. Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ametoa agizo kwa Maafisa Tarafa na Kata kusimamia na kuhamasisha kampeni ya upandaji miti kwenye maeneo yao ili kutunza mazingira.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati akizindua kampeni ya mkoa kupanda miti kwenye barabara na makazi ya watu katika maeneo ya Utengule na Nambogo Manispaa ya Sumbawanga leo .
Katika kuhakikisha kampeni ya urejeshaji uoto wa asili mkoani Rukwa inafanikwa Sendiga amezitaka halmashauri za Nkasi, Manispaa ya Sumbawanga, Kalambo na Sumbawanga kuboresha sheria ndogo ili ziweze kuchua hatua kwa waharibifu wa vyanzo vya maji.
“Maafisa watendaji wa kata zote jukumu lenu ni kwenda kusimamia zoezi la upandaji miti kwenye maeneo yenu. Maafisa Tarafa nendeni pia mkasimamie zoezi hili la upandaji miti Rukwa” alisisitiza Sendiga.
Sendiga alisema mkoa huo una changamoto ya utapiamlo ,hivyo sasa ni wakati wa wananchi kupanda miti ikiwemo ya matunda ili kuimarisha lishe ya familia.
Katika hatua nyingine Sendiga ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Jane Nyamsenda kuhakikisha mitaa ya Manispaa ya Sumbawanga inakuwa safi pamoja na kupandwa miti na maua.
Kwa upande Mwenyekiti wa CCM mkoa Rukwa Silafu Maufi aliyeshiriki zoezi hilo alisema zoezi hilo la upandaji miti lililofanywa na viongozi wa Rukwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwa linapaswa kuwa endelevu.
“Nyumba zote za barabarani zipande miti kuanzia Sumbawanga hadi Tunduma ili kupendezesha mazingira. Miti ni pambo. Vipara vyote juu ya ardhi tuvipande miti” alisema Maufi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Jane Nyamsenda alisema programu ya upandaji miti iliyozinduliwa itakuwa utamaduni kwa wananchi wa Sumbawanga na kuwa itasaidia kurejesha uoto wa asili unaopotea kwa kasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Manispaa ya Sumbawanga ilionesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Desemba 2022 hadi Januari 2023 jumla ya miche 250,190 imepandwa kati ya lengo la miti Milioni Moja na Laki Tano.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato